Trump akosolewa baada ya kuchapisha picha yake akiwa amevaa vazi kama la Papa
-
Trump katika vazi kama la Papa
Rais wa Marekani, Donald Trump, anakabiliwa na shutuma baada ya kuchapisha picha iliyotengenezwa kwa kutumia akili mnemba (AI) inayomuonyesha akiwa amevalia kama papa wa Kanisa Katoliki kwenye jukwaa lake la Truth Social.
Trump amechapisha picha hiyo baada ya kufanya mzaha na waandishi wa habari kwamba angependa kuwa papa ajaye wa Kanisa Katoliki.
Trump alionekana kwenye picha hiyo akiwa amevalia vazi jeupe la papa, na kunyoosha kidole chake cha shahada cha mkono wa kulia kuelekea mbinguni.
Alipoulizwa, nani angependa awe papa ajaye—siku chache kabla ya makadinali kuanza mkutano wao wa faragha kumchagua mrithi wa Papa Francis— Trump alijibu: "Ningependa mimi niwe papa. Hilo lingekuwa chaguo langu la kwanza."
Hata hivyo, Baraza la Wakatoliki la Jimbo la New York, ambalo linadai kuwawakilisha maaskofu wa jimbo hilo katika shughuli zao na serikali, limekosoa vikali picha iliyowekwa na Rais wa Marekani katika mtandao wa kijamii wa Truth Social.
"Hakuna kitu chochote kinachoonesha umahiri au cha kuchekesha kuhusu picha hii, Mheshimiwa Rais," umesema ujumbe wa Baraza la Kikatoliki la Jimbo la New York kwenye akaunti yake ya X.

Ujumbe huo umeongeza kuwa: "Tumetoka kumzika mpendwa wetu, Papa Francis, na makadinali wanakaribia kuingia katika mkutano mkuu wa kumchagua mrithi wa Mtakatifu Petro. Usitufanyie mzaha."
Takriban 20% ya Wamarekani wanajitambulisha kuwa Wakatoliki, na kura za maoni Novemba mwaka jana zilionyesha kuwa karibu 60% kati yao walimpigia kura Trump.
Wakati Trump alipowania urais kwa mara ya kwanza mwaka 2016, na kufanya kampeni akiahadi kujenga ukuta wa mpakani baina ya Marekani na Mexico, Papa Francis alikuwa mmoja wa wakosoaji wake. Papa aliwaambia waandishi wa habari wakati huo kwamba:, "Yeyote, bila kujali ni nani, ambaye anataka kujenga kuta (wa kutenganisha watu) na si madaraja (ya kuwaunganisha), sio Mkristo."