Rais wa Mexico amjibu Trump: Tuko tayari kwa ushirikiano, lakini hatukubali kamwe 'kutiishwa' na US
(last modified Mon, 05 May 2025 10:16:26 GMT )
May 05, 2025 10:16 UTC
  • Rais wa Mexico amjibu Trump: Tuko tayari kwa ushirikiano, lakini hatukubali kamwe 'kutiishwa' na US

Rais wa Mexico Claudia Sheinbaum amekataa pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump la kupeleka wanajeshi ndani ya ardhi ya nchi hiyo kupambana na magenge ya madawa ya kulevya na akasisitiza kwamba, wakati Mexico imeweka mlango wazi kwa ushirikiano, haitakubali kamwe "kutiishwa" kwa Washington.

Sheinbaum ametoa kauli hiyo baada ya ripoti iliyotolewa na gazeti la Wall Street Journal siku ya Jumamosi kudai kwamba, Trump alimshinikiza rais huyo wa Mexico aruhusu Marekani ikatekeleze operesheni za kijeshi ndani ya ardhi ya nchi hiyo.
 
Ripoti hiyo ya Wall Street Journal iliangazia mazungumzo ya katikati ya mwezi Aprili yaliyofanyika kwa njia ya simu kati ya marais wa Marekani na Mexico, ambapoTrump aliripotiwa kushinikiza wanajeshi wa nchi hiyo waruhusiwe kuingia ndani ya ardhi ya Mexico ili wakapambane na magenge ya madawa ya kulevya. Kwa mujibu wa duru za habari, Sheinbaum alipinga vikali wazo hilo na kupelekea kuzuka majibizano makali kati yake na Trump.

Akihutubia katika ufunguzi wa chuo kikuu Rais wa Mexico amethibitisha ripoti hiyo na kuweka wazi msimamo wake.

"Ni kweli" amesema Bi Sheinbaum, na akamnukuu Trump akisema: 'ninapendekeza jeshi la Marekani liingie kusaidia.' Na unajua nilichomwambia? "Hapana, Rais Trump, ardhi yetu haitolewi, mamlaka yetu ya kujitawala hayatolewi, mamlaka yetu ya kujitawala hayauzwi!" 

Rais wa Mexico ameongeza kuwa, ikiwa Trump anataka kusaidia, ajikite katika kuzuia silaha zinazomiminika ndani ya Mexico zikitokea Marekani.../