HAMAS: Jinai za Netanyahu dhidi ya Wapalestina hazitamletea ushindi
(last modified Thu, 15 May 2025 07:38:05 GMT )
May 15, 2025 07:38 UTC
  • HAMAS: Jinai za Netanyahu dhidi ya Wapalestina hazitamletea ushindi

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetangaza kuwa, mashambulizi dhidi ya nyumba za makazi ya watu katika eneo la kaskazini mwa Ukanda wa Gaza yanadhihirisha sisitizo la utawala ghasibu wa Israel kuhusu mauaji ya kimbari ya watu wasio na ulinzi.

Taarifa ya HAMAS imeeleza kuwa, jinai hizo katu hazitaletea ushindi wowote Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu na washirika wake.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) jana Jumatano ilitoa taarifa na kutangaza kuwa, mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni katika nyumba za makazi kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza na kusababisha mauaji ya shahidi zaidi ya watu 70, yanaashiria kuendelea vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wasio na ulinzi.

Harakati ya Hamas imeongeza kuwa: Kushambulia kwa mabomu nyumba za makazi ya watu na kufanya mauaji makubwa dhidi ya wakaazi wasio na ulinzi ni tabia ya kishenzi na ya kifashisti ya utawala wa Kizayuni.

Hamas imeitaka jamii ya kimataifa na nchi za Kiarabu na Kiislamu kuingilia kati kwa kila mbinu ili kuudhibiti utawala wa Kizayuni na kusimamisha vita vya mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza.

Zaidi ya raia 70 ambao wengi wao walikuwa wanawake na watoto waliuawa shahidi na zaidi ya watu 100 walijeruhiwa na kutoweka katika mauaji mapya ya kikatili ya jeshi la Kizayuni katika kambi ya Jabalia kaskazini mwa ukanda wa Gaza.