Uhispania: Tutaendelea kuisaidia UN kifedha kuchunguza jinai za kivita zilizofanywa na Israel Ghaza
(last modified Tue, 06 May 2025 06:40:15 GMT )
May 06, 2025 06:40 UTC
  • Uhispania: Tutaendelea kuisaidia UN kifedha kuchunguza jinai za kivita zilizofanywa na Israel Ghaza

Uhispania itachangia yuro 500,000 (zaidi ya $560,000) kusaidia uchunguzi wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu na uhalifu wa kivita unaowezekana kuwa umefanywa huko Ghaza. Hayo yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania Jose Manuel Albares.

Albares ameiambia Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Uhispania: "kwa lengo la kukomesha ukiukwaji huu wa sheria za kimataifa na kwa nia ya kuhakikisha uwajibikaji, natangaza kwamba tutaiunga mkono Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu katika kuongeza juhudi zake za uchunguzi kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu na uhalifu wa kivita ambao unaweza kuwa umefanywa huko Ghaza". 
 
Ameielezea hali mbaya ya kibinadamu inayoshuhudiwa huko Ghaza kutokana na eneo hilo kuendelea kuwekewa vizuizi na utawala wa Kizayuni wa Israel vya uingizaji misaada ya kibinadamu kuwa "haikubaliki hata kidogo," na kusisitiza kuwaTel Aviv inabeba dhima kwa "kusababisha baa la njaa ambalo halijawahi kushuhudiwa."
 
"Kuingizwa chakula haraka ni muhimu kwa ajili ya kuokoa maisha ya Wapalestina wasio na hatia," ameeleza waziri wa mambo ya nje wa Uhispania na kuongezea kwa kusema: "jamii ya raia wa Ghaza inastahiki utu na amani, na Uhispania inadai hilo na itaendelea kulidai."

Wiki iliyopita, Ismail Thawabteh, mkurugenzi wa ofisi ya vyombo vya habari vya serikali ya Ghaza, alivieleza vyombo vya habari kuwa, eneo hilo limeingia katika "hatua ya juu ya baa la njaa" kutokana na kuendelea kufungwa vivuko vya mpakani na mashambulizi mapya ya kijeshi yanayofanywa na utawala wa Kizayuni.

Zaidi ya Wapalestina 52,500 wengi wao wakiwa wanawake na watoto wameshauawa shahidi hadi sasa katika Ukanda wa Ghaza tangu jeshi la utawala ghasibu wa Israel lilipoanzisha vita vya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya eneo hilo mnamo Oktoba 7, 2023.../