India yaishambulia Pakistan kwa makombora
India imeishambulia Pakistan na hivyo kuibua wasiwasi wa kuzuka vita baina ya mataifa hayo jirani.
India imefyatua makombora kadhaa ndani ya ardhi ya Pakistan mapema leo alfajiri na kusababisha vifo vya watu 8, katika mashambulizi yanayoweza kuzusha vita baina ya nchi hizo mbili jirani na mahasimu wa miaka mingi.
Mamlaka za Pakistan zimesema kuwa, makombora ya India yalililenga jimbo linalozozaniwa na pande hizo mbili la Kashmir pamoja na mkoa wa mashariki wa Punjab. Moja ya makombora liliupiga msikiti kwenye mji wa Bahawalpur na kusababisha kifo cha mtoto mmoja na kujeruhiwa watu wengine kadhaa.
Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif amelaani mashambulizi hayo ya anga na kusema nchi yake inayo haki ya kulipa kisasi kwa hujuma hizo za India alizozitaja kuwa "kitendo cha kivita".
Mzozo wa sasa kati ya India na Pakistan umeibuka baada ya watu waliokuwa na silaha kulifyatulia risasi kundi la watalii katika eneo la kitalii la Pahalgam, lililoko takriban kilomita 90 kutoka Srinagar, mji mkuu wa majira ya joto wa Kashmir inayodhibitiwa na India, na kuua watu wasiopungua 27.
Inafaa kuashiria kuwa India na Pakistan zilitia saini makubaliano ya usitishaji vita mwaka 2003 katika eneo la Kashmir, hata hivyo tangu wakati huo nchi hizo zimekuwa zikiyakiuka makubaliano hayo mara kwa mara. Kashmir ni moja ya maudhui muhimu ambazo nchi mbili zinatofautiana juu yake ambapo kila mojawapo inadai umiliki wake.