Gazeti la Israel: Trump anaweza wikiendi hii akatangaza makubaliano ya kumaliza vita Ghaza
(last modified Fri, 09 May 2025 07:18:50 GMT )
May 09, 2025 07:18 UTC
  • Gazeti la Israel: Trump anaweza wikiendi hii akatangaza makubaliano ya kumaliza vita Ghaza

Rais wa Marekani Donald Trump huenda wikiendi hii akatangaza rasimu ya makubaliano ambayo yatamaliza vita vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza. Hayo yameripotiwa na gazeti la Kizayuni la Israel Hayom.

Gazeti hilo limenukuu duru za kidiplomasia kutoka Marekani na nchi za Kiarabu na kuripotia kuwa, Trump anatarajiwa kutangaza makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo hayatakidhi kikamilifu matakwa ya Israel.
 
Duru za kidiplomasia zilizozungumza na gazeti hilo la Kizayuni zimesema, Trump amefanya mazungumzo mengi kuhusu Ghaza, na kauli zake, kama vile kusema "utajua pengine katika saa 24 zijazo" zinaweza zikawa zinaashiria makubaliano ambayo yataifanya Marekani kuwa na nafasi kuu katika ujenzi na uendeshaji wa Ghaza.
 
Inadaiwa kuwa, katika awamu ya utangulizi ya makubaliano hayo yanayotarajiwa, Marekani itashiriki katika kurejesha misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina waliolazimika kuyahama makazi yao kwa kutumia vituo vya kilojistiki ambavyo jeshi la Israel limeanza kujenga huko Ghaza.
 
Kwa mujibu wa Israel Hayom, hiyo itafuatiwa na "ujenzi upya wa Ukanda wa Ghaza" chini ya uangalizi na usimamizi wa Marekani.
 
Ripoti hiyo imeeleza pia kuwa mstari mwekundu wa harakati ya Palestina ya Hamas juu ya kupokonywa silaha umebaki kuwa moja ya vikwazo vikubwa kwa makubaliano hayo.
 
Hata hivyo kinyume na matakwa yasiyobadilika unayong'ang'ania utawala wa Kizayuni, Hamas inaweza ikapewa dhamana na hakikisho ili iafiki makubaliano hayo, kama vile kushiriki katika siku zijazo kwenye serikali ya kiraia ya Ukanda wa Ghaza na hakikisho la usalama kwa viongozi wake.
 
Uwezekano mwingine uliotajwa ni kuunganishwa Hamas katika vikosi vya Palestina ambavyo vitadhamini usalama katika Ukanda wa Ghaza.
 
Ripoti ya Israel Hayom imebainisha kwamba wasiwasi mkubwa ndani ya serikali ya utawala wa Kizayuni ni kuwa Trump anaweza kutangaza makubaliano ambayo yatalifanya suala la kufikia mwafaka na Hamas kuwa ni jambo lisiloepukika.
 
Aidha imeelezwa kwamba Trump anaweza kuwasilisha makubaliano kwa Israel ambayo ni makubaliano rasmi na yaliyokamilika, na hivyo kumlazimisha waziri mkuu wake Benjamin Netanyahu aamue tu kama anayakubali au la, hali ambayo inaweza kusababisha mgogoro mpya ndani ya muungano wa utawala wake.../