Ufaransa na Uhispania zajadili kuiwekea vikwazo Israel kwa jinai zake Gaza
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa Uhispania wamezungumzia haja ya kuiwekea vikwazo utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kutokana na kuendesha vita vya mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina.
Siku moja baada ya Rais wa Ufaransa kuukosoa utawala ghasibu wa Israel na kuzungumzia haja ya kuchukua hatua dhidi ya Tel Aviv kwa sababu ya ukatili iliofanya huko Gaza, Waziri Mkuu wa Uhispania ameikosoa vikali Israel na kusema, "Hatutaanzisha biashara na Israel inayofanya mauaji ya kimbari," kulingana na kile kilichoripotiwa na tovuti ya Kiebrania Kan.
Shirika la Habari la Bloomberg lilimnukuu Macron akisema kuwa, suala la "kuendelea majadiliano na mikataba ya ushirikiano na Israel jinsi ilivyo" bado ni swali mbele ya madola ya Ulaya.
Rais wa Ufaransa amesema hayo katia mahojiano marefu aliyofanya na TF1, ambapo alijadili masuala ya kigeni na ya ndani. Macron amezungumzia mtazamo wa hivi karibuni wa serikali ya Uholanzi, ambayo inataka kuangaliwa upya kwa pamoja uhusiano wa kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na utawala huo uunaokalia kwa mabavu Palestina.
Akijibu swali kutoka kwa mtazamaji kuhusu kwa nini Ufaransa haikuiwekea vikwazo "Israel," Rais wa Ufaransa alisema, "Hatuwezi kujifanya kuwa hakuna chochote kilichotokea, kwa hivyo ndio ... itabidi kusisitiza shinikizo kwa masuala hayo."
Rais wa Ufaransa pia amemshutumu Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel kwa tabia "isiyokubalika" na "ya aibu" ya kuzuia kuingia misaada kwa Wapalestina huko Gaza.