Sababu za kukatisha tamaa mazungumzo ya simu ya Trump na Putin kuhusu usitishaji vita nchini Ukraine
(last modified Wed, 21 May 2025 11:19:13 GMT )
May 21, 2025 11:19 UTC
  • Sababu za kukatisha tamaa mazungumzo ya simu ya Trump na Putin kuhusu usitishaji vita nchini Ukraine

Kuakisiwa mazungumzo ya simu kati ya Donald Trump na Putin kunaonyesha mfadhaiko na kutiliwa shaka kubwa juhudi za kumaliza vita nchini Ukraine.

Tofauti na yalivyokuwa mazungumzo ya kwanza ya simu ya Trump na Putin, ambayo yaliambatana na tangazo la mpango wa siku thelathini wa amani, mazungumzo ya pili ya simu kati ya viongozi hao yameonyesha kuwepo ubaridi, kusita na hatua zinazochukuliwa na serikali ya Trump kwa ajili ya kuukabidhi mpango huo kwa wahusika wengine, hasa Ulaya.

Trump ameandika kwenye mtandao wa kijamii kwamba vita vya Ukraine ni "tatizo la Ulaya" na kwamba iwapo maendeleo yoyote hayatapatikana, Marekani "itajitenga" na suala hilo zima. Msimamo huo umeibua wasiwasi mkubwa katika miji mikuu mingi ya Ulaya, ambayo ilikuwa ikitarajia kwamba Washington ingechukua jukumu kubwa zaidi katika uwanja huo. Hasa, ikitiliwa maanani kwamba katika mazungumzo hayo Trump hakugusia kutoa mashinikizo yoyote dhidi ya Kremlin wala kifurushi cha pili cha vikwazo bali alielezea tu matumaini yake kwamba hatimaye Putin "atamaliza vita."

Friedrich Mertz, Kansela wa Ujerumani amesema kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba viongozi wa Ulaya wameamua kuongeza mashinikizo dhidi ya Russia kupitia vikwazo baada ya Trump kuwafahamisha kuhusu mazungumzo yake na Putin. Msimamo huu unaonyesha kuwa mazungumzo ya Trump na Putin hayakufanikiwa kufikia lolote.

Ukraine inataka kusitisha mapigano bila masharti yoyote. Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine ambaye awali alikubali wito wa Trump wa kusitisha mapigano mara moja, alizungumza na rais wa Marekani kabla na baada ya wito huo na kusema kuwa iwapo Russia haitasitisha vita itakabiliwa na vikwazo vikali zaidi. Lakini Trump hakuonekana kukubaliana na msimamo huo na pia kumtaja Zelensky kuwa mhusika ambaye si rahisi kuamiliana naye.

Kwa upande mwingine, Russia inataka maeneo inayoyakalia huko Ukraine yatambuliwe rasmi kuwa sehemu ya ardhi yake, suala ambalo linapingwa vikali na Zelensky. Msimamo wa Marekani umesimama juu ya msingi kuwa Ukraine ikubali matakwa ya Russia. Serikali za Ulaya zinaiunga mkono Ukraine dhidi ya Russia.

Putin (kushoto) na Trump

Afisa mmoja wa Ulaya ameiambia Bloomberg kwamba viongozi wa Ulaya wana wasiwasi kwamba Trump ataachana na juhudi za kidiplomasia kuhusu kadhia hiyo. Afisa mwingine ameongeza kuwa Trump ameweka wazi kuwa hayuko tayari kuweka vikwazo vipya na kwamba sasa anajitenga na pendekezo lake mwenyewe la kusitisha mapigano. Kulingana naye, viongozi wa Kiev na mataifa mengine ya Ulaya wanapinga mpango wa Trump wa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Russia na Ukraine.

Huko Russia, simu ya Trump na Putin ilionekana kuwa fursa nzuri ya kusuluhisha mgogoro wa Ukraine. Moscow, ambayo mara zote imekuwa na tahadhari na kutilia shaka ushiriki wa moja kwa moja wa Marekani katika mazungumzo ya amani, sasa inajipata katika hali ambayo inaweza kuchukua hatua katika kuendeleza mazungumzo ya kisiasa bila wasiwasi mkubwa kuhusu vikwazo zaidi au mashinikizo ya kisiasa.

Trump hata amejibu swali kuhusu uwezekano wa Putin kutaka amani kwa kusema, "Labda," suala ambalo limechukuliwa huko Kyiv kuwa alama ya Trump kulegeza msimamo dhidi ya Russia. Zelensky, ambaye amekuwa chini ya mashinikizo ya ndani na nje ya nchi katika wiki za hivi karibuni kuhusu udharura wa kusimamisha vita, ameonya tena kwamba "amani bila kupatikana haki inamaanisha kujisalimisha," na kutaka dhamana ya wazi kutoka kwa nchi za Magharibi kuhusu suala hilo. Lakini sasa, kwa kukosekana uwajibikaji wa Marekani katika uwanja huo, chaguo pekee lililobaki kwa Ukraine ni kuendelea kupambana kwenye medani ya vita, kwa msaada mdogo kutoka kwa washirika wake wa Magharibi. Mawasiliano ya pili kati ya Trump na Putin, kwa maoni ya wachambuzi wengi wa Ulaya, sio hatua kuelekea amani, bali ni kupuuza Marekani majukumu yake katika kuainisha mkondo wa vita. Washington sasa inatekeleza mbinu ya "kukabidhi mgogoro" kwa wengine, kwa kutoa pendekezo la upatanishi wa Vatican na kuamua kukaa kimya mbele ya matakwa ya Kiev kuhusu kuwekwa vikwazo vipya.

Kwa sasa Ulaya haina nguvu ya kijeshi kama Marekani wala uwezo wa kutosha wa kuchochea uhamasishaji wa kidiplomasia. Kuhusiana na hilo, Kremlin inatarajia suala moja tu: Kupita wakati bila shaka kutakuwa ni kwa manufaa ya Russia. Mawasiliano ya pili ya Trump na Putin sio tu hayajaleta amani karibu, bali yameonyesha kuwa matarajio ya kumalizika vita yako mbali zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma.