Uhispania: Kutambuliwa rasmi Palestina ndio njia pekee ya kupatikana amani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania amesema kuwa, nchi yake haina nia ya kutoa nasaha kwa yeyote; lakini njia pekee ya kupata amani ni kuitambua nchi ya Palestina.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania Jose Manuel Albares amesema katika mkutano na mwenzake wa Norway na kubainisha kwamba, Madrid na Oslo zinapaza sauti zaoza kutaka kusitishwa vita huko Gaza ili kutetea haki na utu wa Wapalestina.
Ameongeza kuwa: Tunalichukulia suala la kutetea haki, uadilifu na amani kuwa jukumu letu, na heshima na hadhi ya Ulaya sasa iko katika mtihani huo.
Albares aliendelea kusema kuwa, tumo katika hali ya kuchunguza kuiwekea vikwazo Israel na tunataka msaada wa kibinadamu uingie Gaza bila vikwazo vyovyote.
Ikumbukwe kuwa, juzi Jumamosi Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sánchez alitoa wito wa kuchukuliwa hatua za kimataifa dhidi ya hali "isiyokubalika" huko Gaza na kusisitiza kuwa, Gaza bado itakuwa mali ya Wapalestina na kwamba nchi yake haitanyamaza kimya kuhusu kile kinachoendelea huko.
Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez amewahi kueleza mara kadhaa kwamba, kutambuliwa rasmi taifa la Palestina ni muhimu kwa amani, akisisitiza kwamba hatua ya kuitambua Palestina haijachukuliwa dhidi ya Israel na kwamba ndiyo njia pekee ya kuhakikisha mustakabali wa mataifa mawili yanayoishi bega kwa bega kwa amani na usalama.
Mwishoni mwa mwezi Mei mwaka jana (2024) Uhispania, Ireland na Norway zilipasisha rasmi mpango wa kutambua rasmi Palestina, katika uamuzi ulioratibiwa hatua ambayo imeongeza himaya na uungaji mkono kwa Palestina barani Ulaya.