Brazil: Israel inafanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza
Rais Lula Da Silva wa Brazil amesema kuwa, kinachotokea katika Ukanda wa Gaza Palestina sio vita, ni mauaji ya halaiki.
Kwa mujibu wa Al Jazeera, Luiz Inacio Lula da Silva alisema: "Tunachoshuhudia sasa huko Gaza sio vita hata kidogo kati ya majeshi mawili, bali kuna jeshi moja tu lenye weledi kamili ambalo linaua wanawake na watoto wa Ukanda wa Gaza."
Rais wa Brazil ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za kukomesha mauaji ya halaiki ya Isreal katika Ukanda huo.
Hapo awali Da Silva alikuwa ameishutumu serikali ya Israel, inayoongozwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, kwa kutowajibika kwa kuendelea kufanya mauaji ya raia huko Gaza, na kusisitiza: "Hatuwezi kukaa kimya mbele ya mikengeuko ya Israel (utawala) huko Gaza."
Rais wa Brazil ameongeza kusema kuwa, "Ningependa kutangaza mshikamano na wanawake na watoto wanaoendelea kufa Palestina kutokana na kutowajibika kwa baraza la mawaziri la Israel."
Rais wa Brazil pia aliwahi kulaani mashambulizi ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza katika taarifa zake na kusisitiza kuwa: "Walimwengu hawapaswi kunyamaza kimya mbele ya mauaji yasiyoisha ya Israel dhidi ya Wapalestina."
Hivi karibuni pia, Rais Lula Da Silva wa Brazil sambamba na kulaani mauaji ya watoto tisa wa Dakta Alaa Al-Najjar katika Ukanda wa Gaza yaliyofanywa na Israel alitangaza kuwa, mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni yanalenga kuwafukuza Wapalestina katika ardhi yao.