Mgombea urais Colombia apigwa risasi kwenye mkutano wa kampeni za uchaguzi
Mgombea urais wa Colombia amepigwa risasi tatu wakati akiwa katika hafla ya kampeni katika mji mkuu, Bogota. Miguel Uribe Turbay, (39), alishambuliwa alipokuwa akihutubia umati mdogo katika bustani siku ya Jumamosi.
Polisi walimkamata mshukiwa mwenye umri wa miaka 15 katika eneo la tukio, vyombo vya habari vya eneo hilo vimesema. Mkewe Uribe, Maria Claudia Tarazona, alitoa wito kwa taifa kumuombea ili apone . “Miguel kwa sasa anapigania maisha yake,”. ” Tumuombe Mungu aongoze mikono ya madaktari wanaomhudumia,” alisema. Chama cha Uribe cha Centro Democratico kimelaani shambulizi hilo, kikisema kuwa linahatarisha “demokrasia na uhuru nchini Colombia”.Mashuhuda wa tukio hilo wanasema kuwa, watu wengine wawili pia walijeruhiwa katika tukio hilo.
Serikali ya Colombia imetangaza zawadi ya kitita cha dola 730,000 kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kutiwa mbaroni mtandao uliohusika kuratibu tukio hilo, huku Rais Gustavo Petro akise,a uchunguzi utalenga kubaini ni nani aliyetoa agizo la shambulio hilo.
Turbay ambaye alitangaza nia yake ya kugombea urais kupitia chama cha mrengo wa kulia cha Democratic Center mwezi Machi mwaka huu, alikuwa ameambtana katika mkutano huo na timu ya watu 12 wakati wa tukio hilo. Mwanasiasa huyo alitarajiwa kushiriki uchaguzi wa Rais wa Mei mwakani nchini Colombia. Mama yake aliyekuwa mwanaharakati alitekwa nyara na kuuawa mwaka 1991 wakati wa moja ya vipindi vya machafuko makubwa zaidi katika historia ya Colombia.