Polisi Marekani watumia risasi kuwatawanya waandamanaji Los Angeles
(last modified Mon, 09 Jun 2025 06:58:41 GMT )
Jun 09, 2025 06:58 UTC
  • Polisi Marekani watumia risasi kuwatawanya waandamanaji Los Angeles

Maafisa wa usalama nchini Marekani wametumia gesi ya kutoa machozi na risasi za plastiki katika mji wa Los Angeles siku ya Jumapili, kufuatia hatua ya Rais Donald Trump kupeleka jeshi linalojulikana kama Gadi ya Kitaifa kwa ajili ya kukandamiza maandamano yaliyozuka kupinga dhulma dhidi wahamiaji.

Ghasia hizo, ambazo sasa zimeingia katika siku ya tatu, zilianza baada ya maafisa wa uhamiaji kuwakamata watu kadhaa waliotajwa kuwa wahamiaji haramu.

Misako hiyo iliyofanyika mchana kweupe katika jiji lenye idadi kubwa ya wakaazi wenye asili ya Amerika ya Kusini (Latino) ilisababisha hasira kubwa, hususan kutoka kwa wapigania mageuzi huko Los Angeles.

Wapinzani wa hatua hiyo wamemlaumu Rais Trump kwa kuchochea hali ya taharuki kwa kuamuru kutumwa vikosi hivyo bila ridhaa ya serikali ya jimbo.

Gavana wa California, Gavin Newsom, amelaani vikali uamuzi huo wa Trump akisema, “Hatukuwa na tatizo lolote hadi Rais Trump alipoingilia mambo yetu.” Ameongeza kuwa kitendo hicho ni ukiukaji mkubwa wa mamlaka ya jimbo hilo. Amemtaka Trump kufuta agizo hilo na kurejesha udhibiti wa Gadi ya Kitaifa kwa serikali ya jimbo la California.

Uamuzi wa Rais Trump kuamuru kupelekwa askari wa Gadi ya Kitaifa bila idhini ya jimbo ni jambo adimu. Tukio la mwisho linalokaribiana na hilo lilitokea mwaka 1965, wakati Rais Lyndon B. Johnson alipotuma majeshi kulinda waandamanaji wa haki za kiraia waliokuwa wakitembea kutoka Selma hadi Montgomery, Alabama. Newsom amesema hatua ya Trump ni “ya makusudi yenye lengo la kuchochea hasira,

Jumapili alasiri, waandamanaji walichoma magari matatu  na kuharibu mengine mawili katika eneo la jiji kuu la Los Angeles. Usafiri katika mojawapo ya barabara kuu ulisitishwa kwa zaidi ya saa moja baada ya waandamanaji kufurika barabarani. 

Rais Trump ametetea hatua yake ya kidikteta ya kutuma majeshi hayo, akidokeza uwezekano wa kuipanua kitaifa kwa kutumia Sheria ya Uasi (Insurrection Act), inayoruhusu jeshi kuchukua mamlaka ya kukandamiza maandamano.