Kwa nini wimbi la uungaji mkono kwa Palestina linaongezeka barani Ulaya?
Roma, mji mkuu wa Italia, Jumamosi iliyopita ulishuhudia mojawapo ya maandamano makubwa zaidi dhidi ya Israel barani Ulaya.
Mamia ya maelfu ya makundi ya kiraia, vyama vya mrengo wa kushoto na wanaharakati wa haki za binadamu walishiriki katika maandamano hayo.
Waandamanaji hao wakiwa na picha za hali ya kusikitisha ya watoto huko Gaza, bendera ya Palestina na kupiga nara za kupinga mauaji ya halaiki, walitaka kusitishwa mara moja mashambulizi ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza. Maandamano hayo makubwa yalikuwa tangazo la wazi la kutoridhika umma na sera za serikali ya Giorgia Maloni, Waziri Mkuu wa nchi hiyo.
Licha ya raia kuendelea kuuawa kinyama kila leo na hata kutolewa indhari chungu nzima za mashirika ya Umoja wa Mataifa kuhusu njaa, lakini serikali ya mrengo wa kulia ya Italia imekataa kuchukua msimamo wa wazi dhidi ya hatua za Israel.
Idadi kadhaa ya watu mashuhuri wa kisiasa na kijamii wa Italia walihutubia pambizoni mwa maandamano hayo ambapo huku wakiashiria wajibu wa kimaadili na kihistoria wa Ulaya, walitaka kusitishwa uuzaji wa silaha kwa Israel. Waidha waandamanaji hao walitoa wito wa kusitishwa vita mara moja ili kutuma msaada wa kibinadamu kwa watu waliozingirwa wa Gaza.
Miji mingine mikuu ya Ulaya pia ilikuwa uwanja wa maandamano dhidi ya Israel na uungaji mkono kwa watu wanaodhulumiwa wa Gaza siku ya Jumamosi na Jumapili. Kutoka London hadi Berlin, kutoka Paris hadi Stockholm, raia wa Ulaya waliingia barabarani na kupaza sauti zao za kupinga vita, mzingiro dhidi ya Gaza, njaa na mauaji ya Wapalestina na kutaka sauti zao ziwafikie viongozi wao.

Maandamano hayo yamefanyika kwa kuhudhuriwa na vijana, wasomi, wahamiaji walio wachache na wanaharakati wa haki za binadamu. Maandamano na mikusanyiko katika mitaa ya Ulaya inakinzana waziwazi na mtazamo baridi wa serikali za bara hilo dhidi ya utawala bandia wa Israel.
Mjini London huko Uingereza nako, maelfu ya watu walikusanyika katika viwanja vikuu vya jiji hilo, na shaksia kama vile Jeremy Corbyn, kiongozi wa zamani wa chama tawala cha Labour, walitoa hotuba kali wakitaja vitendo vya Israel kuwa mfano wa uhalifu wa kivita. Huko Berlin Ujerumani pia, licha ya mbinyo mkali wa usalama na mkono wa chuma wa polisi, lakini mikusanyiko mikubwa dhidi ya Israel ilifanyika.
Maoni ya umma ya Ulaya, ambayo yamepata ufahamu wa kina cha maafa ya kibinadamu huko Gaza kupitia vyombo vya habari huru na mitandao ya kijamii, yanataka kubadilishwa mwelekeo wa sera ya kigeni za serikali za Ulaya. Mwenendo huu unaonekana kuongezeka siku baada ya siku.
Matokeo ya uchunguzi wa maoni wa hivi majuzi nchini Ujerumani unaonyesha kuwa, akthari ya raia wanaona kuwa ni makosa kutuma silaha kwa Israel na wanaamini kwamba, serikali inapaswa kuchukua jukumu kubwa katika kusimamisha vita mara moja. Hata hivyo, serikali za Ulaya hadi sasa kwa kiasi kikubwa zimetulia kwa kauli zisizo wazi, kuunga mkono "haki ya kujilinda" ya Israel na ahadi za kibinadamu ambazo kwa hakika hazina athari katika kukomesha vita au kupunguza mateso ya watu wanaodhulumiwa wa Palestina.
Hii ni katika hali ambayo, ripoti zinazoripotiwa kutoka Gaza zinaumiza moyo wa kila mtu ambaye ana ufahamu kidogo juu yake, lakini wapigia upatu haki za binadamu katika nchi za Magharibi wameridhika na kuonyesha majuto tu, kutoa kauli na maneno matupu yasiyoambatana na vitendo na hatimaye kutishia Israel kwamba, wataitambua Palestina kama dola. Tishio ambalo halijawa na athari hata kidogo miongoni mwa Wazayuni.
Ripoti ya mashirika ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu (OCHA) na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu, zinaonyesha kuweko mgogoro wa kibinadamu ambao haujawahi kushuhudiwa huko Gaza.

Takwimu zinaonyesha kuwa, zaidi ya watu 55,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa. Miundombinu ya matibabu imeharibiwa. Njaa imeenea katika Ukanda wa Gaza, na watoto wanakufa kwa utapiamlo. Katika hali kama hiyo, kuendelea kutuma silaha, usaidizi wa kijasusi, au kukaa kimya kuhusiana na operesheni za kijeshi za Israel hakuwezi kuchukuliwa kuwa ni hatua ya kutokuwa upande wowote kwa mtazamo wa sheria za kimataifa na maadili ya kibinadamu.
Kwa kutochukua hatua, serikali za Ulaya zinahalalisha kuendelea kwa ghasia za Wazayuni na hivyo kuzidisha maafa ya kibinadamu huko Gaza.
Nafasi za serikali za Ulaya, haswa Ujerumani, Ufaransa, Uingereza na Italia, zinaonyesha pengo kubwa kati ya maadili yanayodaiwa ya demokrasia ya kiliberali na utendaji wao halisi katika uwanja wa ulimwengu.
Wakati mamilioni ya raia wako mitaani wakitaka mauaji ya halaiki yasitishwe, serikali zao walizozichagua sio tu zinajizuia kuishinikiza Israel, bali zinaongeza ushirikiano wa kijeshi. Mbinu hii ya serikali za Ulaya ni ishara ya mgogoro wa kimaadili, kisiasa na kimuundo katika nchi za Magharibi. Kupuuza matakwa ya umma katika suala lenye misimamo mipana ya kibinadamu na kisheria huko Gaza kumesababisha kudharauliwa kwa madai ya kuheshimu demokrasia na kulinda haki za binadamu ya serikali za Magharibi ndani na nje ya mipaka yao. Leo, Ulaya iko katika mtihani wa kihistoria. Mtihani ambao hautaamua tu mustakabali wa Palestina, bali pia mustakabali wa maadili ya kisiasa katika nchi za Magharibi.
Endapo mgogoro huu utaendelea kupuuzwa namna hii, doa jeusi kwenye uso wa ustaarabu wa Magharibi litabaki milele katika kioo cha historia.