Trump atumia jeshi la wanamaji kukandamiza maandamano Los Angeles
https://parstoday.ir/sw/news/world-i127418-trump_atumia_jeshi_la_wanamaji_kukandamiza_maandamano_los_angeles
Serikali ya rais wa Marekani, Donald Trump, imechukua hatua ya kushangaza kwa kupeleka wanajeshi wa Jeshi la Wanamaji (Marines) jijini Los Angeles ili kuzuia maandamano ya barabarani dhidi ya misako ya wahamiaji, hali ambayo imezua ghadhabu kubwa miongoni mwa umma na kuibua hofu ya mgogoro wa kitaifa.
(last modified 2025-06-10T23:30:43+00:00 )
Jun 10, 2025 23:30 UTC
  • Trump atumia jeshi la wanamaji kukandamiza maandamano Los Angeles

Serikali ya rais wa Marekani, Donald Trump, imechukua hatua ya kushangaza kwa kupeleka wanajeshi wa Jeshi la Wanamaji (Marines) jijini Los Angeles ili kuzuia maandamano ya barabarani dhidi ya misako ya wahamiaji, hali ambayo imezua ghadhabu kubwa miongoni mwa umma na kuibua hofu ya mgogoro wa kitaifa.

Taarifa za vyombo vya habari vya Marekani zinasema kuwa takriban wanamaji 700 kutoka Kusini mwa California walifika Los Angeles Jumatatu usiku kama sehemu ya mkakati wa utawala wa Trump wa kuzuia maandamano hayo.

Jeshi la Marekani lilithibitisha Jumatatu kuwa limeidhinisha kutuma wanajeshi hao kusaidia kuwalinda maafisa wa serikali ya shirikisho na mali zao.

Kamandi ya Kaskazini ya Marekani pia imesema kuwa wanamaji hao, waliwekwa katika hali ya tahadhari mwishoni mwa wiki na waliingia eneo pana la Los Angeles kuanzia tarehe 9 Juni.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Kristi Noem, ameahidi kuendeleza oparesheni kali za kuwakamata wale wanaodaiwa kuvunja sheria za uhamiaji, jambo lililoleta maandamano makubwa katika jiji lenye idadi kubwa ya watu wa asili ya Kilatino.

Wawakilishi wa serikali ya Trump wameeleza maandamano hayo kama ya kihuni, wakilaumu viongozi wa majimbo na miji kutoka chama cha Democrats kwa "kushindwa kudhibiti vurugu" na "kuwalinda wahamiaji haramu kupitia sera za miji salama."

Katika hatua ya kupinga, jimbo la California limeishtaki serikali ya Trump kwa lengo la kuzuia kupelekwa askari wa kikosi cha  Gadi ya Kitaifa kukabiliana na waandamanaji.

Seneta Jack Reed, kiongozi wa juu wa Democrats katika Kamati ya Huduma za Kijeshi ya Seneti, amesema kuwa ameshtushwa kwa kiasi kikubwa na uamuzi wa Trump, akisema: "Rais anatumia nguvu za kijeshi kama silaha ya kisiasa huku akipuuza mamlaka ya gavana na meya, kitendo hiki kisicho na mfano kinaweza kuligeuza jiji kuwa chanzo cha mgogoro wa kitaifa."

Awali Trump aliamuru kutumwa huko Las Angeles wanajeshi 2,000 wa Gadi ya Kitaifa, baada ya kuzuka maandamano yenye vurugu katika baadhi ya maeneo ya mji huo. Ameonya kuwa hataruhusu vikundi alivyoviita kuwa vya majambazi kufanya ghasia mjini na kutatiza utekelezaji wa sheria.