Marufuku ya kutembea usiku yatangazwa Los Angeles. maandamano yaenea Marekani
Watawala wa jiji la Los Angeles wametangaza marufuku ya kutembea usiku katikati mwa jiji hilo ili kudhibiti maandamano yanayochochewa na msako mkali dhidi ya wahamiaji, hali ambayo sasa imeenea hadi miji mingine ya Marekani.
Marufuku hiyo ilitangazwa katika usiku wa tano tangu kuanza machafuko, wakati mamia ya askari wa Jeshi la Wanamaji wa Marekani (Marines) walipowasili katika eneo la Los Angeles siku ya Jumanne, kwa amri ya Rais Donald Trump, hatua iliyoongeza mvutano katika jiji la pili kwa ukubwa nchini humo.
Zikiwa zimesalia dakika tano kabla ya marufuku kuanza kutekelezwa, mamia ya waandamanaji walikuwa wakikabiliana na polisi huku wakiwa wamesimama mikono juu, wakipaza sauti inayosema: “Maandamano ya amani!”
Hatua isiyo ya kawaida ya Rais Trump ya kutuma Kikosi cha Taifa (National Guard) pamoja na askari wa Jeshi la Wanamaji kudhibiti maandamano hayo yaliyotokana na msako wake wa ghafla dhidi ya wahamiaji, imezua taharuki zaidi mjini Los Angeles, na kuchochea maandamano katika miji kadhaa mingine.
Hata baada ya upinzani kutoka kwa viongozi wa mitaa na wa serikali za majimbo, Trump ametuma zaidi ya wanajeshi 4,000 wa Gadi ya Taifa na askari 700 wa Jeshi la Wanamaji Los Angeles.
Polisi wamesema kuwa makundi kadhaa ya waandamanaji waliendelea kuwepo mitaani licha ya marufuku hiyo, na kwamba “kuna operesheni ya kuwakamata kwa wingi .” Polisi pia wameeleza kuwa watu 197 walikamatwa siku ya Jumanne pekee, idadi ambayo imezidi mara mbili jumla ya waliokamatwa siku za nyuma.
Viongozi wa kisiasa wameelezea wasiwasi juu ya kile wanachokiona kama mgogoro wa kitaifa, katika kile kinachotajwa kuwa hatua kali zaidi hadi sasa ya serikali ya Trump katika kampeni yake ya kuwatimua wahamiaji na kukandamiza kwa nguvu wale wanaoandamana kupinga sera zake.
Gavin Newsom, Gavana wa California, katika ujumbe kwa njia ya video amesema: “Hili ni jambo la kutisha , matumizi mabaya ya madaraka na rais aliyeko madarakani yamechochea hali ambayo tayari ilikuwa tete, na kuweka raia wetu, maafisa wa polisi, na hata wanajeshi wa Gadi ya Taifa hatarini."
Amesema 'demokrasia ya Marekani iko mashakani' baada ya Trump kuchochea hali ya mambo kwa kutumia nguvu za kijeshi kukandamiza maandamano. Amebainisha kuwa, huenda California ndiyo ya kwanza, lakini bila shaka haitakuwa ya mwisho kukumbwa na utumiaji mabavu wa Trump.
Maandamano hayo yamesambaa kote nchini Marekani katika miji kama vile Dallas na Austin (Texas), Chicago, na New York, ambako takriban watu elfu moja walikusanyika na waandamanaji kadhaa wakaripotiwa kukamatwa.