Borrell: Mamluki wa Kimarekani wameua Wapalestina 550 huko Gaza katika mwezi mmoja
(last modified Fri, 04 Jul 2025 15:25:29 GMT )
Jul 04, 2025 15:25 UTC
  • Josep Borrell
    Josep Borrell

Mkuu wa zamani wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, amesema kuwa mamluki wa Kimarekani wamewaua Wapalestina 550 huko Gaza katika mwezi mmoja, akishutumu Baraza la Ulaya na Tume ya Ulaya kwa kukaa kimya juu ya matukio hayo.

Katika ujumbe wake kwenye akaunti yake ya X, Josep Borrell mesema, "Katika mwezi mmoja, Wapalestina 550 waliokuwa na njaa waliuawa na mamluki wa Kimarekani walipokuwa wakijaribu kupata chakula katika sehemu za usambazaji zilizoainishwa na Taasisi ya Masuala ya Kibinadamu ya Gaza," ambayo inasimamiwa na Marekani na Israel.

Borrell ameelezea kitendo hicho kuwa cha "kutisha," akilituhumu Baraza la Ulaya na Tume ya Ulaya kwa kutochukua hatua yoyote "dhidi ya uhalifu unaofanywa huko Gaza."

Mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel, ikisaidiwa na nchi kadhaa za Magharibi hususan Marekani, yamesababisha vifo na majeruhi ya zaidi ya Wapalestina 192,000, wengi wao wakiwa watoto na wanawake, na wengine zaidi ya 11,000 hawajulikani waliko. Mamia ya maelfu wamekimbia makazi yao, na njaa inaendelea kuchukua uhai wa Wapalestina wengi, hususan watoto wadogo.