Maprofesa Marekani wafungua kesi dhidi ya kukamatwa wanaounga mkono Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i128064
Kundi la maprofesa nchini Marekani limefungua kesi mahakamani kupinga juhudi za utawala wa Rais Donald Trump za kuwatimua wanafunzi wa kigeni wanaoonyesha msimamo wa kuunga mkono Palestina.
(last modified 2025-07-08T07:52:46+00:00 )
Jul 08, 2025 07:52 UTC
  • Maprofesa Marekani wafungua kesi dhidi ya kukamatwa wanaounga mkono Palestina

Kundi la maprofesa nchini Marekani limefungua kesi mahakamani kupinga juhudi za utawala wa Rais Donald Trump za kuwatimua wanafunzi wa kigeni wanaoonyesha msimamo wa kuunga mkono Palestina.

Maprofesa Marekani wafungua kesi dhidi ya kukamatwa wanaounga mkono Palestina

Kundi la maprofesa nchini Marekani limefungua kesi mahakamani kupinga juhudi za utawala wa Rais Donald Trump za kuwatimua wanafunzi wa kigeni wanaoonyesha msimamo wa kuunga mkono Palestina.

Katika kesi hiyo iliyowasilishwa Jumatatu, walalamikaji wamesema kuwa sera hiyo ya utawala wa Trump imezalisha mazingira ya hofu katika vyuo vikuu, hali iliyowalazimu wanafunzi wengi kunyamaza au hata kuondoka nchini.

Kesi hiyo imewasilishwa na Chama cha Kitaifa cha Maprofesa wa Vyuo Vikuu Marekani (AAUP), ambacho kinawakilisha wasomi kutoka taasisi mashuhuri kama vile Chuo Kikuu cha Harvard.

Walalamikaji wanasema kuwa wanafunzi wanalengwa kwa misingi ya mitazamo yao ya kisiasa, jambo ambalo ni kinyume cha katiba ya Marekani, hasa kifungu cha Kwanza kinacholinda uhuru wa kujieleza.

Kesi hiyo itasikilizwa katika mahakama ya shirikisho huko Massachusetts, ambapo serikali ya Marekani italazimika kutetea msimamo wake kwa mara ya kwanza kuhusu kuwafukuza raia wa kigeni kwa sababu ya maoni yao ya kisiasa.

Kesi hii inafuatia kukamatwa na kuzuiliwa kwa wanafunzi na wasomi kadhaa wa kigeni waliopinga hadharani sera za Marekani zinazounga mkono jinai za Israel dhidi ya Wapalestina.

Serikali ya Marekani inajitetea kwa kusema kuwa uwepo wa watu wanaounga mkono Palestina ni tishio kwa usalama wa taifa. Hata hivyo, wakosoaji wameeleza kuwa hatua hizo zinalenga kukandamiza uhuru wa kisiasa.

Wanafunzi wanaounga mkono Palestina wameendelea kuandamana kupinga vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendeshwa na utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Tangu vita hivyo kuanza tarehe 7 Oktoba 2023, takriban Wapalestina 57,523 wameuawa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto na wengine 136,617 kujeruhiwa. Baaadhi ya takwimu zinaonyesha kuwa Wapalestina waliouawa shahidi katika mauaji hayo ya kimbari ni zaidi ya 100,000/

Katika Chuo Kikuu cha Yale, maandamano ya hivi karibuni ya wanafunzi yalivunjwa kwa nguvu, ambapo wanafunzi 44 walikamatwa na baadhi yao sasa wanakabiliwa na adhabu za kinidhamu.

Vivyo hivyo, Chuo Kikuu cha Tulane kimeanzisha hatua za kinidhamu dhidi ya wanafunzi saba waliokuwa kwenye maandamano ya nje ya chuo wakimtetea Mahmoud Khalil, mwanafunzi wa zamani wa Chuo Kikuu cha Columbia na muandaaji wa maandamano, ambaye anakabiliwa na hatari ya kufukuzwa nchini Marekani.

Tangu Januari, utawala wa Trump umekuwa ukikandamiza wanafunzi wanaoshiriki maandamano ya kuunga mkono Palestina.