Ripoti: Zaidi ya watoto milioni 14 hawakuchanjwa 2024
https://parstoday.ir/sw/news/world-i128352-ripoti_zaidi_ya_watoto_milioni_14_hawakuchanjwa_2024
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, zaidi ya watoto milioni 14 hawakupata chanjo kabisa mwaka jana (2024).
(last modified 2025-07-15T07:19:42+00:00 )
Jul 15, 2025 07:19 UTC
  • Ripoti: Zaidi ya watoto milioni 14 hawakuchanjwa 2024

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, zaidi ya watoto milioni 14 hawakupata chanjo kabisa mwaka jana (2024).

Hayo yamo katika ripoti ya pamoja ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF).

Taarifa ya Pamoja ya UNICEF na WHO iliyolewa leo Jumanne, imeeleza kuwa barani Ulaya na Asia ya Kati, viwango vya wastani vya chanjo ya watoto vilishuka kwa asilimia 1.

Maafisa wameonya kwamba, kuenea kwa habari potofu na kupunguzwa kwa misaada ya kimataifa kunaongeza pengo la chanjo na kuwaweka mamilioni ya watoto hatarini.

Nchi tisa ndiyo zimechangia zaidi ya nusu ya watoto wasiokuwa na chanjo duniani.

Nchi hizo ni pamoja na Nigeria, India, Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Ethiopia, Indonesia, Yemen, Afghanistan, na Angola.

Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, Catherine Russell, amesema kuwa, mamilioni ya watoto bado hawajapata chanjo na hivyo kuwaepushwa na magonjwa yanayoweza kuzuilika, na kwamba jambo hilo linatia wasiwasi.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, mwezi Mei mwaka huu Ethiopia ilitangaza kuwa, imeshawapiga chanjo watoto zaidi ya milioni 11 kama sehemu ya kampeni ya taifa zima ya kudhibiti ugonjwa wa surua unaoendelea kulisumbua taifa hilo.

Kampeni ya chanjo, ambayo imekusudiwa kuwapiga chanjo watoto milioni 17.5 wenye umri wa kati ya miezi tisa hadi miaka mitano, inafanyika hivi sasa katika maeneo yote ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Hayo ni kwa mujibu wa shirika la Fana Broadcasting Corporate ambalo limenukuu taarifa rasmi ya serikali iliyotolewa na maafisa wa Wizara ya Afya wa Ethiopia.