UN: Janga la njaa la Ghaza ni matokeo ya kucheleweshwa upelekaji misaada kwa miezi 22
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130100-un_janga_la_njaa_la_ghaza_ni_matokeo_ya_kucheleweshwa_upelekaji_misaada_kwa_miezi_22
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na uratibu wa masuala ya kibinadamu ametangaza kuwa baa la njaa lililothibitishwa rasmi katika Ukanda wa Ghaza ni matokeo ya kucheleweshwa kwa miezi 22 upelekaji misaada ya kibinadamu katika eneo hilo la Palestina lililowekewa mzingiro na Israel.
(last modified 2025-10-21T09:11:30+00:00 )
Aug 28, 2025 06:07 UTC
  • UN: Janga la njaa la Ghaza ni matokeo ya kucheleweshwa upelekaji misaada kwa miezi 22

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na uratibu wa masuala ya kibinadamu ametangaza kuwa baa la njaa lililothibitishwa rasmi katika Ukanda wa Ghaza ni matokeo ya kucheleweshwa kwa miezi 22 upelekaji misaada ya kibinadamu katika eneo hilo la Palestina lililowekewa mzingiro na Israel.

"Maelfu ya wanawake na watoto huko Ghaza wanakabiliwa na baa la njaa," ameeleza Joyce Msuya wakati akihutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichojadili hali ya mambo katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Mashariki ya Kati jana Jumatano.

"Hakuna mtu katika Ukanda wa Ghaza anayeweza kusalimika na mateso ya njaa", amebainisha Naibu Katibu Mkuu huyo wa UN.

Bi Msuya ameeleza kwamba, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa huko Ghaza kwa sasa ni zaidi ya nusu milioni.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba "njaa katika Ukanda wa Ghaza si matokeo ya ukame au janga la kimaumbile, bali ni jambo lililoratibiwa tokea hapo kabla na matokeo ya miezi 22 ya kukwamishwa misaada ya kibinadamu."

Msuya ametoa indhari pia kwa kusema: "takwimu zinaonyesha kuwa karibu watoto 132,000 huko Ghaza watakumbwa na utapiamlo mkali. Idadi ya watoto wenye njaa wanaokabiliwa na hatari ya kifo imeongezeka mara tatu, na idadi hii inatarajiwa kuongezeka miongoni mwa wanawake wajawazito na wanaonyonyesha".../