Waislamu washerehekea Mazazi ya Mtume (SAW) na Imam Swadiq (AS)
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130630-waislamu_washerehekea_mazazi_ya_mtume_(saw)_na_imam_swadiq_(as)
Wananchi Waislamu wa Iran na baadhi ya nchi za Kiislamu leo Jumatano, inayosadifiana na tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal, wanaadhimisha Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa mbora wa viumbe, Mtume Muhammad (SAW) pamoja na mjukuu wake, Imam Ja'afar bin Muhammad al-Swadiq (AS).
(last modified 2025-09-10T03:11:53+00:00 )
Sep 10, 2025 03:11 UTC
  • Waislamu washerehekea Mazazi ya Mtume (SAW) na Imam Swadiq (AS)

Wananchi Waislamu wa Iran na baadhi ya nchi za Kiislamu leo Jumatano, inayosadifiana na tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal, wanaadhimisha Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa mbora wa viumbe, Mtume Muhammad (SAW) pamoja na mjukuu wake, Imam Ja'afar bin Muhammad al-Swadiq (AS).

Wananchi katika maeneo mbalimbali hapa nchini Iran, wamepamba misikiti, kumbi za masuala ya kiutamaduni, nyumba na mitaa yao kwa maua na taa katika maadhimisho ya kuzaliwa Mtume wa Mwisho na mbora wa viumbe, Muhammad (SAW).

Ushiriki wa Waislamu wa Kishia na Kisuni nchini Iran katika sherehe za Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume (saw) unadhihirisha umoja na mshikamano wa Umma wa Kiislamu.

Sherehe na mahafali za Maulidi zimekuwa zikifanyika kwa siku kadhaa sasa katika misikiti, husainiyya na maeneo mbalimbali ambako washairi, makundi ya qasida na kadhalika yametumbuiza katika vikao na majlisi hizo na kusoma tungo za kumsifu Mtume Muhammad (SAW) na Aali zake watoharifu. 

Waislamu wa madhehebu ya Suni wanaitambua tarehe 12 Rabiul-Awwal kuwa ni siku ya kuzaliwa Mtume (saw) huku wanazuoni wa Waislamu wa madhehebu ya Shia wakisisitiza kuwa, nukuu za kihistoria na hadithi za Maimamu watoharifu katika kizazi cha Mtume (saw) zinaonesha kuwa, alizaliwa tarehe 17 mwezi huu wa Mfunguo Sita Mwaka wa Tembo.

Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imamu Ruhullah Khomeini alitangaza kipindi cha kati ya tarehe hizi mbili (tarehe 12 hadi 17 Rabiul-Awwal) kuwa ni "Wiki ya Umoja baina ya Waislamu" kwa lengo la kuunganisha pamoja Umma wa Kiislamu.

Kwa minasaba hii miwili adhimu ya kuzaliwa Mtume (SAW) na mjukuu wake, Imam Ja'afar al Swadiq (AS), Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mkono wa kheri, baraka na fanaka kwa Waislamu wote duniani hususan wafuasi wa kweli wa Mtume na wapigania haki na uadilifu kote duniani.