Vifo vya malaria kuongezeka kutokana na kupungua misaada
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130688-vifo_vya_malaria_kuongezeka_kutokana_na_kupungua_misaada
Vifo vinavyotokana na ugonjwa wa malaria huenda vikaongezeka mwaka huu kutokana na kupunguzwa kwa misaada ya kigeni.
(last modified 2025-09-11T23:47:47+00:00 )
Sep 11, 2025 23:47 UTC
  • Vifo vya malaria kuongezeka kutokana na kupungua misaada

Vifo vinavyotokana na ugonjwa wa malaria huenda vikaongezeka mwaka huu kutokana na kupunguzwa kwa misaada ya kigeni.

Hayo yameelezwa na mkurugenzi wa taasisi ya Global Fund, yenye makao yake mjini Geneva, Uswisi ambaye ameonya pia kuhusiana na mwenendo unaoongezeka wa kupungua misaada ya kusaidia juhudi za kukabiliana na ugonjwa wa malaria.

Sekta ya afya kwenye mataifa mengi maskini duniani, imetatizika tangu uamuzi wa ghafla wa rais wa Marekani, Donald Trump wa kupunguza ufadhili wa nje wa kifedha.

Wakati nchi nyingine pia tangu wakati huo zimepunguza bajeti zao za misaada ya maendeleo, sekta hiyo imeathiriwa pakubwa ambapo kawaida Marekani ilikuwa mfadhili mkubwa zaidi duniani.

Wataalamu wanasema bara la Afrika ndilo litaathirika pakubwa, ambapo mapambano dhidi ya ugonjwa huo yamekwama katika miaka ya hivi karibuni, kwa kiasi kikubwa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, kuongezeka kwa migogoro, usugu wa dawa na uhaba wa fedha.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kuwa, kwa wastani bara la Afrika linarekodi kesi milioni 200 na vifo 400,000 kwa mwaka vinavyosababishwa na ugonjwa wa malaria. Malaria husababishwa na vimelea na huambukizwa kwa binadamu kupitia mbu jike aina ya Anopheles. Ingawa ugonjwa huo unaweza kuzuilika na kutibika, unaweza kusababisha kifo usipotibiwa.