Uturuki yawapiga marufuku watoto kutumiia mitandao ya kijamii
https://parstoday.ir/sw/news/world-i142100-uturuki_yawapiga_marufuku_watoto_kutumiia_mitandao_ya_kijamii
Serikali ya Uturuki imepiga marufuku kabisa kutoa huduma za mitandao ya kijamii kwa watoto na watu wote wenye umri wa chini ya miaka 15.
(last modified 2026-10-11T03:09:57+00:00 )
Oct 11, 2026 03:09 UTC
  • Uturuki yawapiga marufuku watoto kutumiia mitandao ya kijamii

Serikali ya Uturuki imepiga marufuku kabisa kutoa huduma za mitandao ya kijamii kwa watoto na watu wote wenye umri wa chini ya miaka 15.

Kwa mujibu wa dawati la habari za kimataifa la Shirika la Habari la Tasnim, serikali ya Uturuki imeidhinisha sheria mpya za majukwaa ya mitandao ya kijamii kwa lengo la kuwalinda watoto na vijana wadogo katika ulimwengu wa kidijitali.

Taarifa ya serikali ya Uturuki imesema: "Utoaji wa huduma za mitandao ya kijamii kwa wale walio na umri wa chini ya miaka 15 umepigwa marufuku kabisa. Majukwaa ya mitandao ya kijamii sasa yanatakiwa kuunda matoleo maalumu yenye itifaki zilizoimarishwa za usalama na faragha za watumiaji wenye umri wa miaka 15 hadi 18."

Uraibu wa mitandao ya kijamii ni tatizo linalozidi kuwa kubwa miongoni mwa vijana na watoto katika kona zote za dunia. Tatizo hilo linachochewa na muundo wa kimakusudi wa uraibu wa mitandao ya kijamii. Uchunguzi unaonesha kwamba vijana wengi wanakumbwa na uraibu wa mitandao ya kijamii, wakipata shida kujipapatua nayo licha ya matokeo yake mengi mabaya.

Ishara za wazi zaidi za uraibu wa mitandao ya kijamii ni pamoja na kutumia mitandao hiyo kupita kiasi, kupuuza mahusiano halisi ya kijamii na utendaji duni wa kitaaluma.

Vilevile tafiti kadhaa zimefanyika kuchunguza uhusiano kati ya mitandao ya kijamii na vitendo vya kujiua, hasa miongoni mwa vijana nchini Marekani. Utafiti mmoja uligundua jinsi madaktari katika idara za dharura wanavyoweza kutathmini haraka hali ya afya ya akili ya mgonjwa kwa kutazama akaunti zao za mitandao ya kijamii. Kujiua ni moja ya sababu kuu za vifo kwa vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 24 duniani kote.

Chuo Kikuu cha Utah kiliangazia tatizo la kujiua vijana na kukiri kwamba wazazi ndio wanaopaswa kuwa mstari wa mbele katika kuwalinda watoto wao.