Kundi la RSF laua raia wengine jimboni Kordofan Kaskazini nchini Sudan
Raia wanne wa familia moja wameuawa na wanamgambo wa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka RSF katika jimbo la Kordofan Kaskazini nchini Sudan. Hayo yameripotiwa na kundi huru la kutetea haki za binadamu.
Kundi hilo la 'Emergency Lawyers' limesema, lilirekodi tukio la kuwasili kwa askari wa RSF nyumbani kwa familia hiyo huko Al Mazroub siku ya Jumatatu iliyopita kwa lengo la kupora mali.
Kwa mujibu wa kundi hilo, wanafamilia walipinga jaribio hilo la uporaji kabla ya askari hao kurejea siku iliyofuata na kuua wanafamilia wanne.
Kundi la 'Emergency Lawyers' limelaani mauaji hayo na kuyaelezea kuwa ni "ukiukwaji mkubwa wa haki ya kuishi" na kusema yanaashiria hatari zinazotokana na mashambulizi yanayoendelea dhidi ya raia na mali zao katika mazingira ya kutokuwepo kwa uwajibikaji.
Kundi hilo limetaka ufanyike uchunguzi huru na wa wazi, uwajibikaji kwa wahusika, na hatua za kulinda raia na mali zao.
Mtandao wa Madaktari wa Sudan (Sudan Doctors Network) ulitangaza mnamo Oktoba 3 kwamba raia 25 waliualiwa na wapiganaji wa RSF huko Umm Badr, Kordofan Kaskazini.
Hivi karibuni jeshi la Sudan SAF, limepata mafanikio makubwa ya kijeshi katika sehemu kubwa ya Kordofan Kaskazini kufuatia mapigano na RSF.
Jeshi hilo linakaribia kudhibiti sehemu kubwa ya jimbo hilo, huku maeneo machache, yakiwemo Umm Badr na Jabra Al Sheikh, yakisalia chini ya udhibiti wa kundi hilo la Vikosi vya Usaidizi wa Haraka.
Majimbo matatu ya Kordofan nchini Sudan – Kaskazini, Magharibi, na Kusini – yameshuhudia mapigano makali kati ya jeshi na kundi la RSF tangu tarehe 25 Oktoba mwaka jana.
Sudan imekumbwa na vita vya ndani kati ya jeshi na RSF tangu mwaka 2023 kutokana na kutoelewana kuhusu mpango wa kulijumuisha kundi hilo la wanamgambo katika jeshi rasmi la taifa; hali hiyo imesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu na kuwafanya watu wengine milioni 13 walazimike kuyahama makazi yao…/