UN yawakosoa wanasiasa wanaohujumu Uislamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i14755-un_yawakosoa_wanasiasa_wanaohujumu_uislamu
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amewashambulia wanasiasa wanaohujumu Uislamu kama Donald Trump na mwenzake wa Uholanzi, Geert Wilders akisema kuwa ni walaghai na vidhabadhabina vya kisiasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 06, 2016 11:54 UTC
  • UN yawakosoa wanasiasa wanaohujumu Uislamu

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amewashambulia wanasiasa wanaohujumu Uislamu kama Donald Trump na mwenzake wa Uholanzi, Geert Wilders akisema kuwa ni walaghai na vidhabadhabina vya kisiasa.

Zeid Ra’ad al-Hussein amelaani siasa za kuwahadaa watu na hatari za wanasiasa kama hao na kusema mbinu zinazotumiwa na Donald Trump na Geert Wilders zinashabihiana na zile zinazotumiwa na magaidi wa kundi la Daesh.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema mbinu za kampeni za wanasiasa hao zimesimama juu ya msingi wa kuchochea chuki baina ya watu na kuhubiri sera ambazo zinasababisha dhulma kubwa kwa matabaka mengine ya watu. 

Donald Trump

Mgombea wa kiti cha rais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican, Donald Trump amekuwa akieneza chuki na sera za kibaguzi dhidi ya Waislamu na kutoa wito wa kutumiwa mbinu za dikteta wa zamani wa Ujerumani, Adolph Hitler dhidi ya wafuasi wa dini hiyo. 

Wakati huo huo chama cha Uhuru cha mwanasiasa mwenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia nchini Uholanzi, Geert Wilders kimetangaza kuwa iwapo kitashinda uchaguzi wa mwezi Machi mwakani kitafunga misikiti na shule zote za Kiislamu na kupiga marufuku kitabu kitakatifu cha Qur'ani nchini Uholanzi.