Russia yaitaka Marekani iache kueneza ubabe wake duniani
Waziri wa Ulinzi wa Russia amesema kuwa, Marekani haipaswi kuzilazimisha nchi zingine duniani zifuate sera zake.
Waziri wa Ulinzi wa Russia Sergey Shoigu ametoa kauli hiyo wakati akijibu matamshi ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani Ashton Carter ambaye ameituhumu Moscow kuwa inavuruga mfumo wa kimataifa. Shoigu amesema Marekani ndiyo inayovuruga mfumo wa kimataifa kwa kuzilazimisha nchi zingine zifuate matakwa yake.
Huku akiyataja madai ya Carter kuwa yasiyokuwa na msingi, Shoigu amesema Washington ina dhana potofu kuwa kila kitu kinapaswa kuenda kama inavyotaka. Amesema nchi zote duniani zina haki ya kuamua kuhusu mfumo unapopaswa kufuatwa katika uga wa kimataifa. Shoigu amesema Marekani na waitifaki wake wa nchi za Magharibi wamekuwa wakivuruga mfumo wa kimataifa kuanzia Bosnia, Kosovo, Iraq hadi Libya.
Akizungumza Jumatano iliyopita, katika Chuo Kikuu cha Oxford, Carter aliikosoa vikali Russia na kusema nchi hiyo inavuruga mfumo wa kimataifa sambaba na kujiimarisha kinyuklia.
Waziri wa Ulinzi wa Russia amesema Marekani inapaswa kubadilisha sera zake badala ya kuzilaumu Russia na China kila inaposhindwa kufikia malengo yake kimataifa. Amesema iwapo Marekani itaamua kubadilika, basi masuala kama vile kadhia ya Syria itaweza kutatuliwa.