Mashindano ya Paralimpiki ya Rio De Janeiro Brazil yamalizika
Mashindano ya Olimpiki kwa walemavu yaliyokuwa yakifanyika mjini Rio De Janeiro, nchini Brazil yalimalizika rasmi usiku wa kuamkia leo kwa shamrashamra na nderemo mbalimbali.
Katika michezo hiyo iliyozikutanisha nchi mbalimbali , China imeibuka ya kwanza baada ya kujizolea medali 239. Uingereza imekuwa ya pili katika mashindano hayo ya michezo ya walemavu baada ya kujikusanyia medali 147 huku Ukraine ikishika nafasi ya tatu baada ya kupata medali 117.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilifanya vyema katika mashindano hayo baada ya wawakilishi wake kutwaa jumla ya medali 24 na hivyo kushika nafasi ya 15 katika msimamo wa ugawaji medali hizo.
Kwa upande wa Afrika Mashariki, Kenya inaongoza kwa kubeba jumla ya medali 6 na Uganda Medali 1.
Hata hivyo Iran ilipata pigo katika mashindano hayo baada ya mchezaji wake mwendasha Baisikeli kufariki dunia akiwa mashindano.
Tangazo la kukumbuka kufariki dunia mwanamichezo wa Iran Bahman Golbarnezhad katika hafla ya kufunga mashindano hayo lilileta simnazi kubwa.