Malaysia yataka kupatiwa ufumbuzi matatizo ya Waislamu wa Rohingya
Ahmad Zahid Hamidi Naibu Waziri Mkuu wa Malaysia ametaka kutekelezwa mpango kamili na jumuishi wa kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayowakabili Waislamu wa Rohingya; ambao wamelazimika kuhama Myanmar na kuwa wakimbizi kutokana na mashinikizo ya Mabudha wenye misimamo mikali wa nchi hiyo.
Akihutubia Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Naibu Waziri Mkuu wa Malaysia ameeleza kuwa upo udharura wa kushirikiana Myanmar, Jumuiya ya ASEAN na Umoja wa Mataifa ili kupata suluhisho la tatizo hilo. Ahmad Zahid Hamidi amefafanua kuwa nchi yake imekuwa imewapa hifadhi Waislamu wa Rohingya zaidi ya 150,000 na kuongeza kuwa msaada wa raia hao si tu kuwapatia mahali kwa ajili ya kuishi. Amesema kuwa, Malaysia huwenda ikaweza kuwapa hifadhi Waislamu wa Rohingya kwa muda tu, lakini akasema kuwa ipo haja ya kuwa na mpango kamili na jumuishi utakaokuwa suluhisho la matatizo yanayowasibu Waislamu wa Rohingya. Naibu Waziri Mkuu wa Malaysia ameeleza kuwa kunahitajika msaada wa nchi za kusini mashariki mwa Asia (ASEAN) na vile vile wa Umoja wa Mataifa ili kuisadia Myanmar.
Weledi wa mambo wanaona kuwa mpango kuhusu kadhia ya Waislamu wa Rohingya uliowasilishwa na Malaysia katika Umoja wa Mataifa unaweza kuzingatiwa na kutoa ushawishi kwa kiasi kikubwa katika duru za kimataifa ili kuipatia ufumbuzi kadhia hiyo. Umoja wa Mataifa umewataja Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar kuwa ni jamii ya wachache iliyodhulumika zaidi duniani na kusisitiza kuwa, serikali ya Myanmar inapaswa kuchukua hatua kutatua matatizo ya raia hao. Hii ni kwa sababu serikali ya Myanmar haiwatambui Waislamu wa Rohingya kuwa ni raia wa nchi hiyo, bali inawachukulia kuwa ni wahajiri waliohamia Myanmar kutoka Bangladesh. Sababu hiyo imewafanya Waislamu hao kunyimwa kila haki ya kiraia wanaostahiki kupata kama raia wengine wa Myanmar. Wakati huo huo katika miaka miwili ya hivi karibuni Mabudha wenye misimamo mikali wa Myanmar wamekuwa wakizishambulia nyumba za Waislamu hao na kuwauwa ili kukimaliza kabisa kizazi hicho na hivyo kuwalazimisha raia hao waikimbie nchi yao. Upuuzaji wa serikali ya Myanmar kwa mashambulizi hayo ya Mabudha wa nchi hiyo wenye misimamo ya kufurutu ada umepelekea maelfu ya Waislamu wa Rohingya kuomba hifadhi katika nchi jirani ili kuokoa maisha yao.

Hata kama Waislamu wa Rohingya wanaishi katika kambi za wakimbizi huko Malaysia na katika nchi nyingine za eneo, lakini serikali ya nchi hiyo inaona kuwa suala hilo haliwezi kuwa la kudumu. Hii ni kwa sababu, wakimbizi hao wanaishi katika hali ngumu kwenye kambi hizo ambazo hazina suhula zozote za afya na tiba. Hii ni katika hali ambayo Waislamu wa Rohingya wenyewe wanajitambua kuwa ni Wamyanmar huku wakiamini kuwa nchi hiyo hiyo ni yao na hawastahiki kuishi kama wakimbizi huku watoto wao pia wakinyimwa kila suhula za kielimu. Sababu hiyo imeifanya serikali ya Malaysia iwasilishe Umoja wa Mataifa mpango huo kamili na jumuishi wa wakimbizi ili kuweza kupata uungaji mkono wa duru za kimataifa na kwa njia hiyo waishinikize serikali ya Myanmar itatue matatizo ya raia hao.

Ingawa Aung San Suu Kyi Mshauri wa ngazi ya juu wa serikali na Waziri wa Mambo ya Nje wa Myanmar amebainisha katika Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu mpango wa serikali wa kutatua matatizo ya kimadhehebu huko Myanmar, lakini nchi za eneo ikiwemo Malaysia zimetaka serikali ya Myanmar ionyeshe misimamo ya wazi na ya kiutendaji ili kutanzua mgogoro wa wakimbizi wa Kiislamu wa Rohingya. Serikali ya Malaysia inaamini kuwa, Waislamu wa Rohingya wanaweza kurejea majumbani kwao iwapo serikali ya nchi hiyo itawadhaminia usalama katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo katika mkoa wa Rakhin na wakati huo huo kukabiliana na vitendo vya aina yoyote vya uchupaji mipaka vya Mabudha wa nchi hiyo; na kisha serikali hiyo pia iwaandalie Waislamu hao mazingira na suhula za kimsingi za kuendelea kuishi kwa kuwadhaminia haki zao za kiraia.