Wanachama wa NATO kutoingilia vita vya Uturuki,Russia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i1639-wanachama_wa_nato_kutoingilia_vita_vya_uturuki_russia
Baadhi ya nchi wanachama wa Shirika la Kijeshi la NATO zimetahadharisha kuhusu kushtadi kwa mivutano baina ya Uturuki na Russia na kusisitiza kuwa hazitoingilia endapo vitazuka vita baina ya nchi hizo mbili.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 21, 2016 02:49 UTC
  • Wanachama wa NATO kutoingilia vita vya Uturuki,Russia

Baadhi ya nchi wanachama wa Shirika la Kijeshi la NATO zimetahadharisha kuhusu kushtadi kwa mivutano baina ya Uturuki na Russia na kusisitiza kuwa hazitoingilia endapo vitazuka vita baina ya nchi hizo mbili.

Maafisa wa nchi wanachama wa NATO wamesema wana wasiwasi mkubwa kutokana na kushtadi kwa mivutano tangu Uturuki ilipoitungua ndege ya kivita ya Russia ndani ya ardhi ya Syria.

Aidha wana wasiwasi pia kutokana na kitisho kilichotolewa na Uturuki cha kutuma vikosi vya nchi kavu ndani ya ardhi ya Syria ambako Russia inatekeleza operesheni za mashambulio ya anga dhidi ya makundi ya kigaidi kwa ombi la serikali ya Damascus.

Gazeti la Kijerumani la Der Spiegel limemnukuu Waziri wa Mambo ya Nje wa Luxembourg, Jean Asselborn akisema kuwa NATO haiwezi kukubali kutumbukizwa kwenye ugomvi wa kijeshi na Russia kutokana na mivutano ya karibuni baina ya Moscow na Uturuki.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Luxembourg amefafanua kuwa Ibara ya tano ya Hati ya kuasisiwa NATO inayotoa hakikisho la kuiunga mkono nchi yoyote mwanacama inapokabiliwa na adui wa nje "ina itibari ya kutumika pale tu nchi mwanachama inaposhambuliwa waziwazi".

Gazeti la Der Spiegel aidha limemnukuu mwanadiplomasia mmoja wa Ujerumani ambaye hakutajwa jina lake akisema:"Hatutolipa gharama ya vita vitakavyoanzishwa na Waturuki".

Kufuatia kuongezeka vitisho vya Uturuki vya kushadidisha moto wa machafuko nchini Syria, Russia iliitisha kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kujadili rasimu iliyopendekeza kuhusiana na suala hilo.

Hata hivyo katika kikao cha baraza hilo kilichofanyika siku ya Ijumaa nchi za Magharibi zenye kura ya veto, yaani Marekani, Ufaransa na Uingereza ziliipinga rasimu hiyo iliyopendekezwa na Moscow.../