Wamarekani waanza kuisakama Saudia juu ya shambulio la Septemba 11
https://parstoday.ir/sw/news/world-i16435-wamarekani_waanza_kuisakama_saudia_juu_ya_shambulio_la_septemba_11
Mjane wa Kimarekani ambaye mumewe aliuawa katika shambulizi la Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani ameipeleka mahakamani serikali ya Saudi Arabia kwa kuhusika na hujuma hiyo, sambamba na kutaka kulipwa fidia kutokana na mauaji ya mumewe.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 01, 2016 04:23 UTC
  • Wamarekani waanza kuisakama Saudia juu ya shambulio la Septemba 11

Mjane wa Kimarekani ambaye mumewe aliuawa katika shambulizi la Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani ameipeleka mahakamani serikali ya Saudi Arabia kwa kuhusika na hujuma hiyo, sambamba na kutaka kulipwa fidia kutokana na mauaji ya mumewe.

Stephanie Ross DeSimone, amewasilisha kesi hiyo katika mahakama moja jijini New York, akiutuhumu utawala wa Riyadh kuwa ulifadhili shambulizi hilo linalodaiwa kutekelezwa na kundi la kigaidi la al-Qaeda.

Mjane huyo ameiambia mahakama kwamba alikuwa mjamzito wakati mumewe Patrick Dunn, ambaye alikuwa kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Pentagon alipouawa katika hujuma hiyo ya Septembe 11.

Bunge la Kongresi la Marekani likipigia kura veto ya Rais Obama juu ya shambulizi la 9/11

Hivi karibuni Kongresi ya Marekani ilipiga kura na kubatilisha veto ya Rais Barack Obama wa Marekani kuhusiana na muswada uliopasishwa unaotaka kushtakiwa Saudia kutokana na kuhusika kwake katika shambulio la Septemba 11.

Wawakilishi wa Kongeresi ya Marekani walibatilisha veto hiyo ya Rais Obama iliyopinga muswada huo kwa kura 348 za ndio na 74 za hapana. Aidha Baraza la Seneti la Marekani nalo limepiga kura ya kubatilisha pia kura ya veto ya Rais Obama ambapo wawakilishi 97 wa baraza hilo walipiga kura ya ndio mkabala na kura moja ya hapana.

Rais Barack Obama wa Marekani

Akizungumzia hatua hiyo, Rais Barack Obama amesema kuwa, hatua ya vyombo hivi viwili kupinga turufu yake dhidi ya muswada unaotoa fursa ya Saudi Arabia kushtakiwa kuhusiana na mashambulio ya Septemba 11 imeweka "mfano mbaya na hatari."

Kadhalika utawala wa Aal-Saud umeonya kuwa, kubatilishwa kwa veto ya Rais Obama na Baraza la Seneti na Kongresi ya Marekani kutakuwa na taathira hasi katika uhusiano wa Riyadh na Washington.