Wamarekani wengi wahofia wizi wa kura katika uchaguzi wa rais
https://parstoday.ir/sw/news/world-i16555-wamarekani_wengi_wahofia_wizi_wa_kura_katika_uchaguzi_wa_rais
Wamarekani waliowengi wana hofu kuwa kutajiri wizi wa kura katika uchaguzi wa rais unaotazamiwa kufanyika tarehe 8 mwezi ujao wa Novemba.
(last modified 2025-12-01T10:34:25+00:00 )
Oct 03, 2016 04:01 UTC
  • Wamarekani wengi wahofia wizi wa kura katika uchaguzi wa rais

Wamarekani waliowengi wana hofu kuwa kutajiri wizi wa kura katika uchaguzi wa rais unaotazamiwa kufanyika tarehe 8 mwezi ujao wa Novemba.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni, aslimia 38 ya Wamarekani wanaamini kuwa kutakuwepo na wizi wa kura na uchakachuaji mkubwa katika uchaguzi nchini humo huku 39 wakisema kutakuwa na uchakachuaji japo si mkubwa. Hayo ni kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa na  shirika la habari la Associated Press na Kituo cha Utafiti wa Masuala ya Umma cha NORC.

Uchunguzi huo wa maoni umebaini kuwa idadi kubwa ya wafuasi wa chama cha Republican ndio wanaoamini wizi wa kura utakuwepo wakati wa uchaguzi. Zaidi ya nusu ya Warepublican wanasema kutakuwa na wizi wa kura katika hali ambayo ni robo ya Wademocrat tu ndio wanaoamini uchaguzo huo utakumbwa na dosari na uchakachuaji.

Hillary Clinton na Donald Trump

Aidha asilimia 58 ya wafuasi wa mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump wanaamini kutakuwa na wizi wa kura huku asilimi 18 tu ya wafuasi wa mgombea wa chama cha Democrat, Hillary Clinton,  wakiwa na mtazamo sawa na huo.

Tayari Trump ameshabainisha wasi wasi wake kuwa yamkini uchaguzi wa Novemba ukawa na wizi wa kura. Akizungumza Ijumaa mjini Michigan, Trump alisema wizi wa kura ni tatizo kubwa sana Marekani lakini hakuna anayethubutu kuzungumza kuhusu maudhui hiyo. Katika mdahalo wake na Clinton Jumatatu iliyopita, Trump alisema ana wasi wasi kuhusu uwezekano wa uchaguzi wa Marekani kutokuwa huru na wa haki.