FAO: Chakula na kilimo viende sanjari na mabadiliko ya tabia nchi
Hali ya hewa duniani inabadilika, hivyo uzalishaji wa chakula na kilimo lazima vibadilike pia kwenda sanjari na mabadiliko hayo.
Kauli hiyo imetolewa na mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO katika maadhimisho ya siku ya chakula duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Oktoba 16.
Mkurugenzi wa FAO, José Graziano da Silva amesema kauli mbiu ya mwaka huu ni hali ya hewa inabadilika ,na hivyo ametoa wito kwa nchi zote duniani kujumuisha masuala ya chakula na kilimo katika mipango ya hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Ameongeza kuwa uwekezaji hasa katika maeneo ya vijijini ni muhimu sana ili kudhamini uhakika wa chakula. Amesema, "chakula ni haki ya msingi ya binadamu, lakini bado kuna watu karibu milioni 800 wanaokabiliwa na njaa duniani kote, bila uhakika wa chakula. Amesema malengo ya maendeleo endelevu hayawezi kufikiwa, ndio maana ajenda ya mwaka 2030 inatoa wito wa kutokomeza njaa pamoja na kuchangia kilimo endelevu.
Mkuu wa FAO ameonya kuwa, malengo haya ni bayana yako hatarini kwani wakati mabadiliko ya hali ya hewa yakiendelea, tayari yanaathiri rutuba kwenye udongo, misitu, bahari, maeneo ambayo ni tegemeo kwa sekta ya kilimo na uhakika wa chakula. Ameongeza kuwa wahanga wakubwa ni wakulima wadogowadogo wanaoishi katika maeneo ya vijijini kwenye nchi zinazoendelea, ambao hawana nyenzo za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.