UN yaeleza matumaini yake kuhusu makubaliano ya kisiasa DRC
https://parstoday.ir/sw/news/world-i17815-un_yaeleza_matumaini_yake_kuhusu_makubaliano_ya_kisiasa_drc
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesema ana wingi wa matumaini kuwa makubaliano ya kisiasa yaliyofikiwa Jumanne iliyopita katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yatasaidia kuheshimiwa haki za binadamu sambamba na kufanyika uchaguzi wenye itibari katika nchi hiyo ya Kiafrika.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Oct 20, 2016 10:18 UTC
  • UN yaeleza matumaini yake kuhusu makubaliano ya kisiasa DRC

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesema ana wingi wa matumaini kuwa makubaliano ya kisiasa yaliyofikiwa Jumanne iliyopita katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yatasaidia kuheshimiwa haki za binadamu sambamba na kufanyika uchaguzi wenye itibari katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Ban Ki-moon amesema makubaliano hayo kati ya chama tawala na baadhi ya vyama vya upinzani huenda yakatoa mwanga wa kisiasa na kuleta anga nzuri ya kuheshimiwa haki za binadamu, mambo ambayo anaamini yatapelekea kufanyika uchaguzi huru, wa haki na wa kidemokrasia mnamo Aprili mwaka 2018.

Kadhalika Katibu Mkuu wa UN ameitaka serikali ya Rais Joseph Kabila iendelee kujenga muamala na mazingira mazuri ya kuvishawishi vyama vingine vya siasa ambavyo havikutia saini makubaliano hayo ya kisiasa, viunge mkono juhudi hizo kwa maslahi ya amani, utulivu na mustakabali mwema wa kisiasa nchini humo.

Rais Joseph Kabila wa DRC

Hali ya taharuki ingali imetanda katika miji kadhaa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hususan mji mkuu Kinshasa, huku wafanyakazi wa sekta mbalimbali wakisusia kazi kufuatia wito wa wapinzani wanaopinga makubaliano ya kisiasa yaliyofikiwa  Jumanne.

Jean-Marc Kabund-a-Kabund, katibu wa chama kikuu cha upinzani cha Umoja kwa Ajili ya Demokrasia na Maendeleo ya Kijamii nchini humo amesema kuwa, chama hicho hakiyatambui makubaliano ya kisiasa yaliyotiwa saini baina ya washiriki wa mazungumzo ya kisiasa huko Kinshasa, mji mkuu wa nchi hiyo.

Maandamano dhidi ya serikali mjini Kinshasa mwezi jana, ambapo watu 50 waliuawa

Viongozi wa chama tawala nchini Kongo DR wanadai kuwa, kutokana na changamoto za kilojistiki, ni vigumu kuitisha uchaguzi wa rais ndani ya mwaka huu; huku wapinzani wakisisitiza kuwa makubaliano hayo ya kisiasa yamempa Rais Kabila ambaye muhula wake wa pili unamalizika Disemba mwaka huu, nafasi ya kuendelea kusalia madarakani kwa muda wa mwaka mmoja na nusu zaidi.