Syria: Magaidi wanazuia raia kutoka mji wa Aleppo
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa amesema wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh wanawazuia raia kuugura mji wa Aleppo, ambao kwa sasa unashuhudia makabiliano makali kati ya vikosi vya serikali na magenge ya kigaidi.
Bashar al-Jaafari, Balozi wa kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa aliyasema hayo jana katika mkutano wa Baraza Kuu la umoja huo na kuongeza kuwa, Damascus imetengeneza njia nane za kutoka mji wa Aleppo; sita kwa ajili ya raia na mbili kwa ajili ya magaidi ambao wako tayari kujisalimisha kwa serikali. Hata hivyo amesema makundi ya kigaidi ya Jabhatu Nusra na Ahrar al-Sham yamefunga njia za kutoka raia katika mji huo.
Jaafari ameongeza kuwa, mapema jana magaidi hao waliwaua kwa kuwakata vichwa watu 14 waliokuwa wakiwashawishi wananchi kuondoka katika mji huo na kwamba matakfiri hao wanatumia raia kama ngao katika mashambulizi yao. Aidha magaidi hao wametishia kuyateketeza moto majumba ya watu watakaoukimbia mji wa Aleppo.
Jeshi la Syria likisaidiwa na vikosi vya jeshi la anga la Russia hivi karibuni lilianzisha operesheni kubwa ya kijeshi kwa minajili ya kuwatimua magaidi katika mji wa Aleppo na hadi sasa magaidi wa Daesh na wa makundi mengine ya kigaidi zaidi ya 1000 wameuliwa na wengine karibu 2500 kujeruhiwa.
Balozi wa kudumu wa Syria katika UN ameongeza kuwa, hadi kufikia sasa watu zaidi ya milioni moja na laki saba wamefanikiwa kuyakimbia maeneo ambayo ni ngome za magenge hayo ya kigaidi na kukimbilia maeneo salama ambayo yako chini ya serikali, magharibi mwa nchi.