IOM: Wakimbizi 410 wamefariki dunia wakiingia Ulaya 2016
Wakimbizi na wahajiri wapatao 410 wamepoteza maisha mwaka huu wa 2016 wakijaribu kuingia Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranea.
Shirika la Kimataifa la Uhajiri (IOM) limetoa taarifa na kuongeza kuwa wakimbizi 102,547 wameingia Ulaya kupitia Ugiriki huku wengine 7,507 wakiingia Ulaya kupitia Italia tangu mwanzo wa mwaka huu wa 2016.
Taarifa hiyo imesema karibu nusu ya wakimbizi hao ni raia wa Syria na wengine ni kutoka Afghanistan na Iraq.
Wakati huo huo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limetahadharisha kuwa, kufungwa mipaka ya nchi za Ulaya kutapelekea kuvurugika zaidi hali ya wakimbizi barani humo.
Msemaji wa UNHCR Karin de Gruijl, pia amekosoa hatua ya Macedonia kufunga mipaka yake na kuwabagua wakimbizi.
Mwaka 2015 karibu wakimbizi milioni moja waliingia Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranea huku wengine 3,700 wakipoteza maisha au kutoweka katika safari hiyo hatari. Aghalabu ya wakimbizi hao wanakimbia vita vinavyoendelea Syria na Iraq.