Wakimbizi 700 waokolewa katika bahari ya Medditerranean
Gadi ya ulinzi wa fukweni ya Italia imetangaza habari ya kuokolewa wakimbizi zaidi ya 700 katika bahari ya Mediterranean.
Gazeti la Le Figaro la Ufaransa limeinukuu gadi ya ulinzi wa ufukweni ya Italia ikitangaza leo kuwa, wakimbizi 729 wameokolewa katika bahari ya Mediterranean na kuwapeleka katika bandari ya Catane iliyoko katika kisiwa cha Sicily nchini Italia.
Gadi ya ulinzi wa fukweni nchini Italia imesisitiza kuwa, zaidi ya watu laki sita waliokuwa wamepanda boti kadhaa, wameokolewa katika kipindi cha baina ya siku za Ijumaa na Jumapili.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wakimbizi laki moja na 55 elfu wameokolewa tangu mwanzoni mwa mwaka huu katika bahari ya Mediterranean.
Matteo Renzi, Waziri Mkuu wa Italia alisema jana kuwa, nchi hiyo haina uwezo wa kukabiliana na wimbi la wakimbizi wanaoivamia nchi hiyo tangu mwaka jana.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Wakimbizi (OIM), zaidi ya wakimbizi laki tatu na 500 wamekimbilia barani Ulaya tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi hivi sasa kupitia bahari ya Mediterranean.