Mogherini: Trump hana uwezo wa kubatilisha JCPOA
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 hayawezi kubatilishwa na serikali moja kwa kuwa yana baraka kamili ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Akiongea hapo jana katika mkutano usio rasmi wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Federica Mogherini amesema ni kwa maslahi ya EU na Umoja wa Mataifa UN, kutekelezwa kikamilifu makubaliano hayo yaliyopewa jina Mpango Kamili wa Utekelezwaji JCPOA na kwamba yeye binafsi alitwikwa jukumu la kuhakikisha kuwa hayakiukwi.
Mbali na suala la makubaliano hayo ya nyuklia ya Iran yaliyofikiwa Julai mwaka jana na kuanza kutekelezwa Januari mwaka huu, mawaziri hao wa Umoja wa Ulaya wamejadili taathira zinazotegemewa katika mabadiliko ya sera za kigeni za Marekani, kufuatia ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa rais wa Marekani.
Rais mteule wa Marekani Donald Trump aliwahi kusema wakati wa kampeni kuwa, mapatano ya nyuklia ya Iran ni 'maafa na mapatano mabaya zaidi duniani' na kuahidi kuyachana katika siku yake ya kwanza katika Ikulu ya White House.
Hata hivyo katika hatua inayoonekana ni ya kulegeza msimamo, Walid Phares, mshauri wa Trump katika masuala ya sera za kigeni akizungumza baada ya ushindi wa mwanasiasa huyo wa Republican katika uchaguzi wa Marekani, alisema kunapaswa kufanyika mazungumzo ya kutathmini upya mapatano hayo.