UN yaainisha tarehe ya kujiondoa rasmi Gambia ICC
Umoja wa Mataifa umetangaza tarehe ya kujiondoa rasmi Gambia katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.
Farhan Haq, Msemaji wa UN amesema Gambia itaacha kuwa mwanachama wa Mkataba wa Roma uliobuni mahakama hiyo ya mjini The Hague kuanzia Novemba 10 mwaka ujao 2017.
Mwezi uliopita wa Oktoba, Gambia ilijiunga na orodha ya nchi kadhaa za Afrika zilizotangaza azma yao ya kujiondoa katika Mkataba wa Roma uliobuni ICC Julai mwaka 2002.
Sheriff Bojang, Waziri wa Habari wa Gambia alisema nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika inaazimia kujiondoa ICC kutokana na kile alichokitaja kuwa, mahakama hiyo iliyoko mjini The Hague nchini Uholanzi inatumika kuwahujumu na kuwadhalilisha viongozi wa Afrika.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda hivi karibuni bila kusema iwapo Uganda itafuata mkondo huo, aliipongeza Afrika Kusini, Burundi na Gambia kwa kuanzisha mchakato wa kujiondoa katika Mkataba wa Roma.
Nchi kadhaa za Kiafrika zimetishia kujiondoa kwenye mahakama hiyo kutokana na hatua yake ya kuendelea kuwasakama viongozi wa nchi za bara hilo, huku ikifumbia macho jinai zinazofanywa na viongozi wa Magharibi.