Trump aonywa asiugeuze urais kuwa mali ya ukoo wake
Taasisi moja ya kusimamia masuala ya maadili nchini Marekani imetoa onyo kali dhidi ya Donald Trump, rais mteule wa nchi hiyo na huku ikiashiria kuwa urais si mali ya ukoo, imemtaka aache kuwaingiza wanawawe katika siasa za Marekani.
Gazeti la USA Today limemnukuu Fred Wertheimer mkuu wa kundi la kusimamia masuala ya kimaadili linalojulikana kwa jina la Democracy 21 akimtaka Donald Trump aache kabisa kuingiza wanawe katika masuala ya siasa za Marekani.
Amesema, haikubaliki kabisa kujiingiza watoto wa Trump katika masuala ya kisiasa na kwamba rais huyo mteule wa Marekani anapaswa kufikiria upya mara moja misimamo yake kuhusu suala hilo.
Mwito huo wa kundi la Democracy 21 ambalo ni la kuangalia maadili ya viongozi wa Marekani na masuala yanayohusu kuvunjwa haki za raia umekuja baada ya Donald Trump kutaka wanawe wapewe hadhi kubwa ya watu ambao wana uwezo wa kupata nyaraka za siri kabisa za taifa, jambo ambalo ni kinyume na maadili ya kisiasa nchini Marekani.
Baadhi ya vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa, Donald Trump ana nia ya kuwatoa wanawe katika masuala ya biashara na kuwafanya kuwa washauri wa usalama wa taifa.
Hadi hivi sasa maandamano dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa Marekani yanaendelea huku waandamanaji wakipiga nara wakisema, Trump si rais tuliyemchagua sisi.