Uchunguzi: Marekani ilishinikiza kutimuliwa kamanda wa Kenya, Sudan Kusini
Uchunguzi uliofanywa na shirika moja la kimataifa la kutathmini masuala ya sera umefichua kuwa, Marekani ilishinikiza kufutwa kazi kamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Kenya aliyekuwa akisimamia Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani nchini Sudan Kusini (UNMISS).
Ripoti ya uchunguzi uliofanywa na shirika la International Policy Group imebainisha kuwa, uamuzi wa Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kumtimua Luteni Jenerali Johnson Mogoa Kimani Ondieki raia wa Kenya ambaye alikuwa anaongoza operesheni za UNMISS ulikuwa wa kisiasa na uliolenga kuikingia kifua serikali ya Washington kwa kushindwa kuwadhaminia usalama raia wake walioko Sudan Kusini.
Uchunguzi wa shirika hilo umesema kuwa, raia wa Marekani walihujumiwa na kudhalilishwa kwa makusudi, wakati yalipoanza mapigano mapya mjini Juba kati ya Julai 8 na 25. Ripoti ya International Policy Group imeutaka Umoja wa Mataifa kuiomba radhi Kenya pamoja na kamanda wake huyo aliyetimuliwa Sudan Kusini, sambamba na kumtaka Luteni Jenerali Johnson Ondieki kutafuta haki kwa kuishtaki UN katika mahakama ya kimataifa.
Kadhalika ripoti hiyo imependekeza kuwa, wakati umefika kukibadilisha Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani nchini Sudan Kusini (UNMISS) na kile cha Kikosi cha Afrika cha Kulinda Amani Sudan Kusini (AMISS).
Hii ni katika hali ambayo, tayari Kenya imeanza kuwaondoa askari wake waliokuwa wakihudumu katika kikosi cha UNAMISS, hatua iliyochukuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kulalamikia hatua ya Ban kutimua kamanda wa Kenya na nafasi yake kupawa raia wa China.