Waislamu wa Myanmar waandamwa na mateso ya kila upande
Waislamu wa kabila la Rohingya wa nchini Myanmar waliokuwa wanakimbilia nchini Bangladesh kwa ajili ya kuokoa maisha yao kutokana na mauaji wanayofanyiwa na askari wa serikali ya mabudha nchini mwao, sasa wanazuia na gadi ya nchi kavu Bangladesh wasiingie tena nchini humo.
Taarifa zinasema kuwa, askari wa gadi ya ulinzi wa mpaka, wamewazuia Waislamu 125 wa Rohingya kuingia Bangladesh licha ya kushtadi mauaji dhidi yao. Kwa mujibu wa habari hiyo, miongoni mwa Waislamu hao 125, 61 ni wanawake na 36 ni watoto wadogo. Waislamu hao wa Myanmar walikuwa ndani ya mitumbwi saba katika maji ya mto Naf unaoitenganisha Bangladesh na Myanmar. Jumamosi ya jana vyombo vya serikali ya Myanmar vilitoa ripoti yenye mgongano kuhusu habari hiyo.
Inafaa kuashiria kuwa, Kuna Waislamu milioni 1.1 nchini Myanmar na wengi wao wanaishi katika jimbo lenye machafuko la Rakhine. Wailamu hao wanakumbwa na vitendo vya mara kwa mara vya ukatili kutoka kwa mabudha. Katika jinai ya hivi karibuni kabisa, Waislamu zaidi ya 30 wameuawa kwenye jimbo la Rakhine. Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, jamii ya Waislamu wa kabila la Rohingya, ndiyo jamii ya wachache inayoongoza kwa kudhulumiwa duniani. Jamii hiyo inaunda asilimia nne ya raia wote wa Myanmar.