Malaysia: Makumi ya raia waliojiunga na ISIS wameuawa na magaidi wenzao
Khalid Abubakar, Kamanda wa Upelelezi wa jeshi la Polisi nchini Malaysia amesema kuwa, zaidi ya raia 50 wa nchi hiyo waliokuwa wamejiunga na kundi la ukufurishaji la Daesh wameuawa na wanachama wa genge hilo.
Kwa mujibu wa Khalid Abubakar, raia hao wa Malaysia wameuawa wakati wakijaribu kutoroka ili kurejea makwao kutoka mataifa ya Syria na Iraq walikokwenda kujiunga na makundi hatari ya kigaidi baada ya kurubuniwa. Abubakar ameyasema hayo kupitia hotuba aliyoitoa katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Kimataifa nchini Malaysia. Kamanda wa Upelelezi wa jeshi la Polisi nchini Malaysia amesema kuwa wakati wa kujiunga na genge hilo baadhi ya raia wa nchi hiyo walichana au kuzichoma moto pasi na vitambulisho vyao na kwamba wale watakaorejea nchini watapata msamaha wa serikali kwa ajili ya kuanza maisha yao ya kawaida.

Hata hivyo amesema kuwa, Wamalaysia na Indonesia waliojiunga na kundi hilo la ukufurishaji wamekuwa wakiuawa kwa wingi kila pale wanapotaka kuachana na magenge ya kigaidi ili kurejea makwao. Waindonesia na Wamalaysia wengi waliorubuniwa na kujiunga na magaidi wa Kiwahabi wako nchini Iraq na Syria wakipigana bega kwa bega na wanachama wa magenge ya ukufurishaji dhidi ya serikali halali za mataifa hayo. Hayo yanajiri kufuatia makundi ya kigaidi kupata pigo huko Iraq na Syria, baada ya majeshi ya nchi hizo kutekeleza operesheni kali dhidi yao na hivyo kufelisha njama chafu za mabwana zao hususan Marekani, Israel, Saudia, Qatar na Uturuki.