Trump: Mshindi wa uchaguzi kwa kura za wananchi ni mimi
Rais mteule wa Marekani Donald Trump amesema matokeo rasmi ya uchaguzi wa rais wa nchi hiyo yamejumuisha pia kura zisizo halali na kwamba zikiwekwa kando kura hizo yeye ndiye mshindi wa uchaguzi huo.
Bilionea huyo wa Marekani aliibuka mshindi katika uchaguzi wa rais wa Marekani baada ya kushinda kura za wajumbe wa majimbo zaidi ya 270 yanayohitajika kumwezesha mgombea kushinda uchaguzi huo.
"Mbali na kupata ushindi mkubwa wa kura za wajumbe nilishinda pia kura za wananchi ikiwa utaweka kando mamilioni ya watu ambao walipiga kura kinyume cha sheria", amedai Trump bila ya kutoa ushahidi wowote.
Hii ni katika hali ambayo majumuisho ya karibuni ya kura za wananchi katika uchaguzi wa rais wa Marekani uliofanyika tarehe 8 ya mwezi huu wa Novemba yanaonyesha kuwa mpinzani wake Trump, Bi Hillary Clinton, ameshinda kwa zaidi ya kura milioni mbili huku idadi hiyo ikitazamiwa kufikia kura milioni mbili na nusu.
Ushindi huo mkubwa wa Clinton katika kura za wananchi umezusha malalamiko makubwa dhidi ya mfumo wa uchaguzi wa rais nchini Marekani ambapo maandamano ya kupinga ushindi wa Trump yamefanyika katika majimbo mbalimbali ya nchi hiyo.
Rais mteule wa Marekani ametoa kauli ya kudai alishinda pia katika kura za wananchi baada ya timu ya kampeni ya Bi Hillary Clinton kutangaza siku ya Jumamosi kuwa imekubali kushiriki kwenye zoezi la kuhesabu tena kura katika jimbo la Wisconsin kufuatia ombi lililowasilishwa na Jill Stein, mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Kijani. Trump ameuelezea kuwa ni "dhihaka" uamuzi huo wa kuhesabiwa tena kura za jimbo hilo.../