Makampuni makubwa ya teknolojia yakataa kushirikiana na Trump katika kuwajasisi Waislamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i21496-makampuni_makubwa_ya_teknolojia_yakataa_kushirikiana_na_trump_katika_kuwajasisi_waislamu
Wafanyakazi wa makampuni makubwa ya teknolojia ya Marekani yamekataa kushiriki katika sera zinazopiga vita Uislamu na wahamiaji za rais mteule wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 16, 2016 00:05 UTC
  • Makampuni makubwa ya teknolojia yakataa kushirikiana na Trump katika kuwajasisi Waislamu

Wafanyakazi wa makampuni makubwa ya teknolojia ya Marekani yamekataa kushiriki katika sera zinazopiga vita Uislamu na wahamiaji za rais mteule wa nchi hiyo.

Zaidi ya wafanyakazi 200 wa makampuni makubwa ya teknolojia ya Marekani ikiwemo kampuni ya Alphabet, Twitter na Salesforce yametangaza kuwa hayatashirikiana na serikali ya Donald Trump katika kujasisi wateja wao kwa mujibu wa imani na itikadi zao za kidini.

Makampuni hayo pia yamekataa kuwafukuza au kuwaachisha kazi wahamiaji.

Risala iliyotiwa saini na wafanyakazi hao imesema: Tutasimama bega kwa bega na Waislamu wa Marekani, wahajiri na watu wote ambao maisha yao yanahatarishwa na serikali mpya.

Makampuni ya teknolojia kutumiwa kwa ajili ya ujasusi dhidi ya Waislamu Marekani

Wakati wa kampeni zake za uchaguzi, rais mteule wa Marekani, Donald Trump alizungumzia masuala mengi yanayohusiana na wahamiaji, Waislamu na mikakati ya kujasisi na kufuatilia nyendo za Waislamu kupitia makampuni ya teknolojia, suala ambalo limezusha mjadala mkubwa ndani na nje ya Marekani. 

Wiki chache zilizopita pia Trump alisema kuwa, anakusudia kuwateuwa watu muhimu ambao watamsaidia kutekeleza mipango ya usimamizi wa serikali na kuzitia msimbo data, taarifa na habari zinazohusiana na Waislamu na wahamiaji, suala ambalo limezitia wasiwasi mkubwa kampuni za teknolojia.

Kwa msingi huo wakurugenzi wa makampuni makubwa ya teknolojia ya mawasiliano kama Apple, Amazon Com, Alphabet, na Facebook wanatazamiwa kukutana na timu ya rais mteule wa Marekani, Donald Trump.