Kuzidi kunyanyaswa wakimbizi barani Ulaya na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i21724-kuzidi_kunyanyaswa_wakimbizi_barani_ulaya_na_marekani
Vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wageni na wakimbizi vimeshika kasi katika nchi za Ulaya na Marekani kufuatia nchi hizo kuweka sheria kali za kuwadhibiti wahamiaji na wakimbizi wanaokimbilia nchi hizo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 19, 2016 07:44 UTC
  • Kuzidi kunyanyaswa wakimbizi barani Ulaya na Marekani

Vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wageni na wakimbizi vimeshika kasi katika nchi za Ulaya na Marekani kufuatia nchi hizo kuweka sheria kali za kuwadhibiti wahamiaji na wakimbizi wanaokimbilia nchi hizo.

Ikiwa ni kuendelea na misimamo yao isiyo ya kibinadamu dhidi ya wageni na wakimbizi, nchi za Ulaya na Marekani zimechukua hatua kali ikiwa ni pamoja na kufunga kambi za wakimbizi na kuwarejesha walikotoka wakimbizi hao bila ya kujali mazingira ya nchi zao. Hivi sasa serikali ya Uingereza imekataa ombi la Ufarana la kupokea watoto elfu mbili wa wakimbizi ambao wamekosa pa kwenda baada ya Ufaransa kufunga kambi ya wakimbizi ya Calais. Serikali ya Ujerumaini nayo imetangaza kuwa, zaidi ya wakimbizi elfu tatu wa Afghanistan ambao wameshindwa kupata hati ya ukimbizi nchini humo, watarejeshwa nchini kwao. Ndege kadhaa zimetengwa kwa ajili ya kuwarejesha mjini Kabul, wakimbizi hao waliokataliwa na Ujerumani. Ikiwa ni kuendeleza siasa hizo zisizo za kibinadamu, bunge la Uswisi nalo limepitisha sheria mpya za kuwabana wageni na wakimbizi wanaokimbilia nchi za Ulaya.

Sehemu kubwa ya nchi za Ulaya zimekataa kupokea wakimbizi kwa kiwango kilichoainishwa na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR. Baadhi ya nchi za Ulaya kama vile Ujerumaini zilijifanya ni wema na zenye huruma sana kwa wakimbizi, mwanzoni mwa kuanza mgogoro katika nchi za Mashariki ya Kati hususan vita vya Iraq na Syria. Viongozi hao wa Ujerumaini walitoa majigambo mengi ya kupigania haki za binadamu na hata kutangaza hadharani kuwa inawakaribisha kwa mikono miwili wakimbizi, lakini hivi sasa imebadilika kikamilifu na imeamua kufanya siasa kali dhidi ya ya wakimbizi. Baadhi ya nchi za Ulaya zimefunga kikamilifu mipaka yao licha ya kwamba wakimbizi wengi wanateseka vibaya kwenye mipaka ya nchi hizo.

Wakimbizi wengi hupoteza maisha yao wanapokuwa njia kuelekea barani Ulaya

 

Wakimbizi wengi na hususan watoto wadogo na wanawake, wanatekwa nyara na magenge ya kimafia na kuwatumia vibaya. Baadhi ya nchi za Ulaya zinaamua kuonesha wazi chuki zao dhidi ya wageni na wakimbizi kutoka eneo la Mashariki ya Kati. Wakati nchi  hizo zikiwanyanyasa na kuwabagua wakimbizi hao kutoka Mashariki ya Kati, wanawafungulia milango na kuwapokea kwa mapana na marefu wahajiri kutoka Ukraine. Nchini Poland pia hali ni hiyo hiyo. Serikali ya nchi hiyo inafanya ubaguzi wa wazi baina ya wakimbizi; inawanyanyasa wakimbizi Waislamu na kulegeza kamba mbele ya wakimbizi Wakristo. Siasa za Umoja wa Ulaya nazo ni kuzuia wakimbizi kuvuka mipaka ya nchi za Ulaya.

Kwa mujibu wa makublaiano yaliyofikiwa baina ya Umoja wa Ulaya na Uturuki, nchi za umoja huo zimejitolea kuilipa Uturuki fedha nyingi ili izuie kuingia barani Ulaya wakimbizi wa Syria na Iraq. Umoja wa Ulaya umewekeana mkataba kama huo pia na baadhi ya nchi za kaskazini mwa Afrika kama vile Tunisia na Niger. Jambo la kusikitisha ni kuona kuwa, ni nchi za Ulaya na Marekani ndizo zilizosababisha matatizo yote haya yanayozitesa nchi za Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika kuanzia kuziweka madarakani na kuziunga mkono tawala za kidikteta hadi kuunda magenge ya kigaidi, kuyapa silaha na kuyasaidia kwa njia mbalimbali magenge hayo katika jinai zao zilizowafanya wakazi wa maeneo hayo ambao kabla ya kuvamiwa na magenge ya kigaidi walikuwa wakiishi kwa utulivu na amani na hawakuwa na fikra kabisa ya kuyakimbia maeneo yao.

Wananchi wakiandamana dhidi ya ubaguzi nchini Marekani

 

Siasa za kibaguzi na unyanyasaji dhidi ya wageni zimeshamiri pia huko nchini Marekani hasa baada ya kutangazwa Donald Trump kuwa mshindi wa uchaguzi wa hivi karibuni wa Rais. Jana Jumapili, wananchi wa Marekani walifanya maandamano makubwa katika Siku ya Kimataifa ya Wahajiri dhidi ya sera na siasa za kibaguzi za rais mteule wa nchi hiyo zinazopiga vita wahamiaji. Maandamano hayo yalifanyika mjini New York mbele ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa sambamba na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wahajiri. Wamarekani wanaowaunga mkono wahajiri walielekea katika jumba la rais mteule wa nchi hiyo, Donald Trump kupinga siasa na mitazamo ya kiongozi huyo inayowabagua na kuwapiga vita wahamiaji.

Kiujumla ni kwamba miamala isiyo sahihi ya nchi za Ulaya na Marekani dhidi ya wakimbizi na wahamiaji imezifanya taasisi za kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa kulalamika na jambo hilo linazidi kuondoa pazia lililofunika vitendo visivyo vya kibinadamu vinavyofanywa na madola ya Ulaya na Marekani ambayo yanajilabu na kujigamba kuwa ni watetezi wakuu wa haki za binadamu duniani.