EU, Arab League zalaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni
Umoja wa Ulaya EU na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zimelaani hatua ya utawala ghasibu wa Israel kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.
Taarifa ya pamoja ya EU na Arab League iliyotolewa jana Jumanne katika mji mkuu wa Misri, Cairo baada ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, imesema kuna udharura wa utawala haramu wa Israel kusitisha ujenzi huo haramu, kughusubu ardhi na kubomoa nyumba za Wapalestina.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, sera ya kughusubu ardhi ya Israel, kukiwemo kukalia kwa mabavu Quds Tukufu, sambamba na kubomoa makazi ya Wapalestina, inakiuka sheria za kimataifa na kwamba vitendo hivyo ni kizingiti katika mchakato wa amani.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wamesisitiza kuwa, jamii ya kimataifa ina jukumu la kushirikiana na wadau wote kuhakikisha kuwa inahitimisha kukaliwa kwa mabavu ardhi za Wapalestina kunakofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel tangu mwaka 1967.
Haya yanajiri siku chache baada ya Nikolay Mladenov Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Mashariki ya Kati kulaani uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa kujenga nyumba mpya za walowezi wa Kiyahudi zipatazo 500, huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan hususan mashariki mwa Baitul Muqaddas; na kuutaka utawala huo kusitisha hatua zake hizo zilizo kinyume cha sheria. Israel ililivamia na kulikalia kwa mabavu eneo la Baitul Muqaddas ya mashariki mwaka 1967 ambayo ni ardhi ya Palestina; hatua ambayo imepingwa na kulaaniwa na jamii ya kimataifa.
Kwa sasa Bunge la Israel (Knesste) linajadili muswada wa kuidhinisha ujenzi wa nyumba mpya 4000 katika Ukingo wa Magharibi, hatua ambayo imelalamikiwa vikali na Umoja wa Mataifa.