Ulaya: Trump weka wazi siasa zako za masuala ya kigeni
https://parstoday.ir/sw/news/world-i23935-ulaya_trump_weka_wazi_siasa_zako_za_masuala_ya_kigeni
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumini, Ursula Gertrud von der Leyen amemtaka Donald Trump, rais mteule wa Marekani aweke wazi siasa zake za mambo ya kigeni hasa baada ya kujitokeza matamshi ya kugongana baina ya viongozi wa serikali ijayo ya Marekani kuhusu Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi, NATO.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 20, 2017 06:45 UTC
  • Donald Trump, rais mteule wa Marekani
    Donald Trump, rais mteule wa Marekani

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumini, Ursula Gertrud von der Leyen amemtaka Donald Trump, rais mteule wa Marekani aweke wazi siasa zake za mambo ya kigeni hasa baada ya kujitokeza matamshi ya kugongana baina ya viongozi wa serikali ijayo ya Marekani kuhusu Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi, NATO.

Viongozi wa nchi za Ulaya wamekasirishwa na misimamo ya hivi karibuni ya Trump kuhusu uhusiano wa siku za usoni wa Marekani na nchi za Ulaya hususan katika masuala ya ulinzi na usalama, na hasa matamshi yaliyotolewa na Trump siku ya Jumatatu ambapo aliwalaumu wanachama wa NATO kwa kushindwa kutenga fedha za kuendeshea shirika hilo. Hasira kubwa zinaonekana waziwazi katika matamshi ya viongozi wa ngazi za juu wa Ulaya. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amekiri kuwa matamshi hayo ya Trump kuhusiana na NATO yamewakasirisha viongozi wa Ulaya na kuzitaka nchi hizo kufikiria kuimarisha zenyewe usalama na ulinzi wao. Kwa kweli nchi za Ulaya zinaelewa vyema kwamba, kutokana na kuitegemea Marekani kwa miongo mingi katika upande wa ulinzi na usalama hususan katika suala la kudhamini sehemu kubwa ya bajeti ya NATO, iwapo kutatokea mabadiliko ya ghafla, jambo hilo litakuwa na madhara makubwa katika upande wa kiulinzi wa nchi za Ulaya na litazusha mivutano mipya kati ya nchi za bara hilo hususan kuhusu mchango wa kila nchi wa kudhamini bajeti ya NATO na pia bajeti ya masuala ya kijeshi ya Umoja wa Ulaya.

Bendera za NATO na Marekani

 

Jambo ambalo limewafanya viongozi wa Ulaya wachanganyikiwe zaidi ni matamshi yanayogongana ya viongozi wapya wa Marekani. Hivi sasa Donald Trump analikosoa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO kutokana na matatizo yake mengi kama kutokuwa na uwiano mzuri wa kimuundo,  kikazi na majukumu ya kila mwanachama na kusisitiza kuwa, NATO imepoteza falsafa ya kuundwa kwake na ndio maana inabuni maadui na hatari za uongo mara kwa mara ili kujilinda isivunjike. Hata hivyo, James Martin, aliyependekezwa na Donald Trump kushika nafasi ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani ana mtazamo tofauti. Martin ametoa matamshi tofauti na ya Donald Trump kuhusiana na NATO na kusema kuwa nchi za Ulaya ni waitifaki wazuri wa Washington na hiyo ni rasilimali kubwa ya kiistratijia kwa Marekani. Amesema, Marekani inahitajia muungamano wa kimataifa ili iweze kufanikiwa katika siasa zake. Pia amedai kuwa, NATO ni jumuiya iliyofanikiwa sana katika historia ya zama hizi au pengine katika historia nzima ya mwanadamu. Kwa mtazamo wa Martin, Marekani inapaswa kuimarisha zaidi na zaidi uhusiano wake wa kijeshi na kiusalama na nchi za Ulaya.

Ursula Gertrud von der Leyen, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani

 

Kwa kuzingatia hayo tutaona ni jinsi gani viongozi wapya wa Marekani wanavyokinzana kwenye misimamo yao hata kabla ya kuingia madarakani. Tena mgongano huo unaonekana kwenye masuala muhimu na makubwa yaani masuala ya kiulinzi na siasa za nje za Marekani. Kuweko migongano hiyo mikubwa kati ya viongozi wapya wa Marekani kumewafanya viongozi wa Ulaya kuitaka Marekani iweke wazi misimamo yake hususan kuhusu Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, halitakuwa jambo rahisi kuondoa migongano hiyo katika serikali ijayo ya Marekani hasa kwa kuzingatia misimamo ya Donald Trump, rais mteule wa Marekani. Hivyo kinachotarajiwa ni kuongezeka misuguano hiyo ndani ya serikali ijayo ya Marekani hususan kama Trump na Waziri wa Ulinzi ajaye wa Marekani hawatokuwa tayari kubadilisha misimamo yao.