Myanmar yakaidi mwito wa OIC wa kukomesha jinai dhidi ya Waislamu
Serikali ya Myanmar imepuuza mwito uliotolewa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) mjini Kuala Lumpur, nchini Malaysia hivi karibuni, wa kutaka ikomeshe mauaji, ukandamizaji na jinai za kutisha dhidi ya Waislamu wa Rohingya. Wizara ya Mambo ya Nje ya Myanmar jana Jumamosi ilitoa taarifa ya kuikashifu vikali serikali ya Malaysia kwa kuwa mwenyeji wa kikao cha dharura cha OIC cha kujadili hali ya Waislamu wa Myanmar.
Akizungumza katika kikao hicho siku chache zilizopita, Waziri Mkuu wa Mayalsia, Najib Razak alisema kwa miaka mingi sasa Waislamu wa eneo la Rakhine wamekuwa wakikabiliwa na matatizo makubwa na kwamba, bila shaka kutofuatiliwa suala hilo kunatishia usalama na amani ya eneo. Kikao cha dharura cha OIC kilihudhuriwa na wawakilishi wa nchi 57 wanachama wa jumuiya hiyo.
Tangu mwaka 2012 Mabudha wenye misimamo mikali wakisaidiwa na maafisa usalama wa Myanmar wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali za ukatili, mauaji na hata kubaka wanawake Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini humo, mbali na kunyimwa uraia Waislamu wa jamii ya Rohingya wapatao milioni 1.1.