UN, EU, Vatican zakasirishwa na sheria ya ubaguzi ya Trump
https://parstoday.ir/sw/news/world-i24587-un_eu_vatican_zakasirishwa_na_sheria_ya_ubaguzi_ya_trump
Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Vatican zimelaani sheria tata ya ubaguzi ya Rais Donald Trump wa Marekani, ya kuzuia wakimbizi na raia wa nchi saba za Kiislamu kuingia nchini humo.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Feb 02, 2017 04:02 UTC
  • UN, EU, Vatican zakasirishwa na sheria ya ubaguzi ya Trump

Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Vatican zimelaani sheria tata ya ubaguzi ya Rais Donald Trump wa Marekani, ya kuzuia wakimbizi na raia wa nchi saba za Kiislamu kuingia nchini humo.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa jana Jumatano alisema kuwa, sera hiyo ya Washington ya kuzuia wakimbizi haswa wa Syria kuingia nchini Marekani inafaa kufutwa mara moja. Akiongea na waandishi wa habari katika makao makuu ya UN mjini New York baada ya kurejea kutoka mkutano wa Umoja wa Afrika huko Addis Ababa Ethiopia, Gutteres amesema: "Kuwapokea wakimbizi ni suluhu ya haraka na inayotekelezeka kwa wepesi, kwa kuwa wakimbizi ni watu wanaotoroka migogoro na mauaji katika nchi zao."

Wakati huo huo, akihutubia Bunge la Umoja wa Ulaya jana Jumatano kuhusu sheria hiyo ya kibaguzi ya Trump, Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Nje wa EU alisema kuwa, umoja huo unapinga vikali utekelezwaji wa sheria hiyo iliyosainiwa Januari 27, ambapo US imesimamisha mpango wa kuwapokea wakimbizi kwa muda wa siku 120, na vilevile kuzuia kuingia nchini humo raia kutoka nchi sita za Kiislamu, ambazo ni Iran, Iraq, Syria, Yemen, Sudan, Libya na Somalia kwa kipindi cha siku 90.

Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Nje wa EU

Mogherini amebainisha kuwa: "EU haitamzuia yeyote kustafidi na sheria ya ulinzi wa kimataifa wa wakimbizi, tutaendelea kusimamia suala hilo. Tunafurahia kuanguka kwa kuta na kujengwa madaraja."

Huku hayo yakiarifiwa, Askofu Mkuu Angelo Becciu, afisa wa ngazi za juu katika Sektretariati ya Mambo ya Nje ya Makao Makuu ya Kanisa Katoliki Vatican, ameeleza wasi wasi wake kuhusu sheria hiyo ya Trump, akisisitiza kuwa: "Sisi ni wajumbe wa tamaduni tofauti, ule wa kufunguka na kupokea, na muhimu zaidi, kutangamana na wageni wanaokuja katika jamii na tamaduni zetu."

Maandamano ya kupinga ubaguzi wa Trump yaendelea Marekani

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch na Amnesty International pamoja na serikali za nchi zilizopigwa marufuku kuingia Marekani zimekosoa vikali sheria hiyo ya kibaguzi ya Trump.