Wahajiri wengine 1,300 waokolewa katika bahari ya Mediterania
Vikosi vya doria katika pwani ya Italia vimetangaza kuwa vimewaokoa wahajiri 1,300 katika bahari ya Mediterania.
Taarifa iliyotolewa na vikosi hivyo vya doria katika pwani ya Italia imeeleza kuwa wahajiri hao waliokolewa hapo jana katikati ya bahari ya Mideterania katika operesheni 13 tofauti zilizofanywa na timu za vikosi hivyo, vikosi vya wanamaji wa Italia na Uingereza, meli za biashara na meli za mashirika yasiyo ya kiserikali.
Ripoti zinaeleza kuwa jumla ya wahajiri 2,600 waliokuwa katika hatari ya kuzama wameokelewa kwenye bahari ya Mediterania katika kipindi cha siku tatu zilizopita.
Njia ya majini kutokea Libya kuelekea Italia katika bahari ya Mediterania ni moja ya njia kuu zinazotumiwa na wahajiri wa Kiafrika kuelekea barani Ulaya.
Wahajiri 181,000 waliwasili nchini Italia mwaka jana kupitia bahari ya Mediterania, akthari yao wakiwa wameondokea nchini Libya. Mashirika ya misaada yanakadiria watu zaidi ya 5,000 walifariki dunia mwaka uliomalizika wa 2016 katika jitihada za kuingia barani Ulaya…/