Wanaharakati US wawafunza wahajiri njia za kupambana na siasa za Trump
Wanaharakati wa kijamii nchini Marekani, wameanzisha utaratibu wa kuwapatia mafunzo wahajiri haramu juu ya namna ya kupambana na siasa zilizo dhidi ya wahajiri za Rais Donald Trump wa nchi hiyo.
Asasi mbalimbali zinazowatetea wahajiri mjini New York na maeneo mengine ya Marekani zimefanya vikao vya mafunzo ya ushauri kwa wahajiri wenye wasiwasi wa kutimuliwa kutoka Marekani.
Katika vikao hivyo, asasi hizo zimewafunza wahajiri haramu njia wanazotakiwa kuzitumia pindi wanapokutana na maafisa wa uhamiaji wa nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kutowafungulia milango maafisa hao wa uhamiaji.
Imeongeza kuwa, endapo watatiwa mbaroni wasitoe maelezo yoyote bila ya kushauriana na mawakili wao isipokuwa majina yao tu na wasitie saini karatasi ya aina yoyote ile.
Asasi hizo zinasema, maafisa wa serikali ya Marekani hawawezi kumfukuza mtu yeyote nchini humo bila ya kuthibitisha kwamba, anishi nchini humo kinyume cha sheia.
Lengo la vikao vya asasi hizo zinazowatetea wahajiri nchini Marekani na ambavyo vimepewa jina la 'Tambueni Sheria Zenu' ni kufany maandalizi kwa ajili ya kupambana na siasa kali dhidi ya wahajiri ambazo zinatekelezwa na serikali ya Rais Donald Trump.
Wanaharakati hao wanaamini kuwa, kuzingatiwa maelekezo hayo kutasaidia kuwapunguzia wahajiri matatizo yanayowakabili nchini humo kutoka Idara ya Uhamaji na Forodha. Mafunzo kama hayo yametolewa pia katika miji ya New Mexico na Texas.